Na Anna Nkinda –
Maelezo
18/12/2014
VIJANA wametakiwa kujiunga na vikundi vya kuweka akiba na kukopa ili kuchangia mawazo yao na ubunifu na wakati huo huo wanajitengenezea
mazingira ya kujiajiri kwani wengi wao wana elimu na ujuzi walioupata masomoni lakini wanakabiliwa na tatizo la ukosefu
wa ajira.
Rai hiyo imetolewa leo
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua Umoja wa Vikundi vya kuweka
Akiba vilivyopo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wilaya ya
Kinondoni (UWAMAKI) katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Usafirishaji jijini
Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema kupitia vikundi hivyo vijana wanaweza
kupata mitaji midogomidogo pamoja na mafunzo ya kuwawezesha kuanzisha biashara
na kujiajiri. Kwani mfumo huo wa vikundi na mafunzo ni moja ya njia za
kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na hivyo kupunguza tatizo la ajira.
Kwa upande wa wanachama
wa UWAMAKI aliwasisitiza kutoridhika na
mafanikio waliyoyapata bali waendelee kutafuta njia za kupiga hatua hususani kupata
utaalamu wa kuboresha bidhaa zao , kutafuta masoko zaidi na kufanya ubunifu wa
kuweza kuvumbua bidhaa na biashara nyingine tofauti ili kuepukana na ushindani
wa soko.
“Mnapokuwa na bidhaa
zinazofanana mtakuwa katika mazingira ya kushindania soko jambo ambalo litapunguza
kiasi cha mauzo ambayo ndiyo pato lenu wajasiriamali. Jitihada ifanywe ili
kuweza kutafuta watalaam ambao watawapa mafunzo ya kukuza biashara”, alisema
Mama Kikwete.
Akisoma risala ya
vikundi hivyo Katibu wa UWAMAKI , Mwajuma Waziri aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa
kuwawezesha kuwa na vikundi na kupata
mafunzo ya kuweka akiba, elimu ya kibenki, usindikaji wa vyakula na huduma ya
bima ya afya.
Waziri alisema, “Kutokana
na mafunzo hayo tunaweza kuanzisha miradi mbalimbali kama vile kutengeneza
sabuni za maji za kufulia, sabuni za kuoshea vyombo na kusafishia tairizi, siagi
ya karanga na batiki na hatimaye tumeweza kufungua akaunti yetu ya Umoja katika
benki ya wanawake (TWB)”.
Katibu huyo alisema
walianza na kikundi kimoja kwa kujiwekea hisa moja kwa thamani ya shilingi 1000
pia waliweza kukopesha kiasi cha shilingi 6,300,000 mpaka mwisho wa mwaka walivuna
shilingi 12,750,000.
“Hadi sasa tunavikundi
11 vyenye wanachama 274 kati ya hao wanaume ni wanane katika vikundi hivi tumeweza kukopesha kiasi cha shilingi
47,500,000/= na kufikia mavuno ya shilingi 79,739,000 kwa mwaka”, alisema.
Alimalizia kwa kusema
lengo la kuunda umoja huo ni kushirikiana katika matatizo ya kijamii, kuunda
SACCOS na kutafuta masoko ya bidhaa zao.
Taasisi ya WAMA
inasimamia mradi wa kuwawezesha wanawake kwa kuwapa mafunzo kupitia vikundi katika
mikoa ya Dar es Salaam Lindi na Pwani hadi
kufikia Septemba mwaka huu jumla ya watu 18,000 wamefikiwa kwa kupitia vikundi
688 vilivyoundwa na tayari shilingi milioni 227 zimekusanywa na kukopeshwa.
No comments:
Post a Comment