Na
Beatrice Lyimo- Maelezo-DSM
SERIKALI za
Tanzania na Marekani zimetiliana saini kwa ajili ya kuandaa miradi katika sekta ya nishati
itakayofadhiliwa katika Awamu ya pili ya Mkataba wa Millennium Challenge Corporation
(MCC).
Utiaji saini wa mkataba
huo ulifanyika katika Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam ambapo Makamu wa
Rais wa MCC Bw. Kamran Khan
anayeshughulikia Mikataba na Uendeshaji wake pamoja na Waziri wa Fedha wa Tanzania , Mhe. Saada Mkuya ukishuhudiwa
na Balozi wa Marekani nchini Mark Childress.
Akiongea wakati wa
hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya alisema
kuwa MCC imeipatia Serikali ya Tanzania shilingi bilioni 17 kwa ajili ya
utekelezaji wa mradi wa MCC II ambapo mraadi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa
hapo mwakani ukiwa na lengo la kusaidia miundombinu ya umeme nchini.
Makubaliano hayo ni
muendelezo wa ubia imara kati ya Marekani na Tanzania kati ya mwaka 2008 na
2013 ambapo MCC ilitekeleza mkataba wa miradi mikubwa ya uwekezaji katika sekta
za maji, barabara, na nishati ya umeme nchini.
Miradi hiyo iligharimu
jumla ya Dola za kimarekani milioni 698, chini ya mkataba huo mtandao wa nyaya
za umeme wenye zaidi ya kilometa 3,000 ulijengwa.
Kwa kuzingatia
mafanikio hayo katika utekelezaji wa wa programu zilizokuwa chini ya mkataba wa
kwanza kuwahi kutolewa na MCC, taasisi hiyo iliichagua tena Tanzania kuingia
katika mkataba wa pili utakaolenga sekta ya Nishati katika miundombinu pamoja
na mageuzi ya kisera na mifumo ya udhibiti na kitaasisi.
Aidha, upembuzi yakinifu
utaiwezesha Tanzania kuandaa miradi itakayoleta mageuzi katika sekta ya Nishati
ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji wa shirika la ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO)
na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) katika maeneo ya kiufundi, usimamizi wa
fedha na uendeshaji na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme
katika maeneo ya vijijini.
Shirika la Changamoto
za Milenia (MCC) ni Taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi
zinazoendelea, shughuli zake zinajengwa katika misingi kwamba msaada utaleta
ufanisi na matokeo makubwa pale unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi
na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umaskini.
No comments:
Post a Comment