TANGAZO


Friday, November 21, 2014

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani kufanyika Kitaifa mkoani Njombe

 Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Fatma Mrisho akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani yatakayofanyika kitaifa mkoani Njombe kuanzia Novemba 24, 2014 na kufikia kilele chake Desemba 1, 2014.
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Fatma Mrisho akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani isemayo, Tanzania Bila Maambukizi Mapya ya VVU, Vifo vitokanavyo na Ukimwi na Ubaguzi na Unyanyapaa inawezekana inayolenga kupunguza maambukizi Mapya ya Ukimwi, kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi na kukomesha vitendo vya unyanyapaa kwa asilimia Sifuri.
 Mkurugenzi wa ufuatiliaji wa Tathmini wa Ofisi ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi  Tanzania (TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu utoaji wa huduma na upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi kwa watu wanaoishi na VVU katika maeneo mbalimbali nchini.
 Moja ya bango linaloonesha takwimu za hali ya maabukizi ya VVU katika mikoa mbalimbali nchini. Takwimu hizo zilizokusanywa mwaka 2011/2012 zinaonyesha  kuwa mkoa wa Njombe unaongoza kwa kuwa na maabukizi mengi zaidi ukifuatiwa na Iringa, Mbeya na Shinyanga.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa TACAIDS akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mbinu na elimu inayotolewa na TACAIDS katika maeneo mbalimbali ikiwemo matumizi ya mipira ya kike kwa wanawake ili kuzuia maambukizi mapya ya VVU. (Picha na Aron Msigwa - MAELEZO)

Na Beatrice Lyimo na Aron Msigwa- MAELEZO
21/11/2014 .Dar es Salaam.
MAADHIMISHO ya siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka 2014 kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Njombe kuanzia tarehe 24 mwezi huu hadi tarehe  moja Desemba. 
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya tume hiyo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mrisho amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Tanzania bila maambukizo mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Vifo vitokanavyo na UKIMWI, Ubaguzi na unyanyapaa inawezekana.
“Kauli mbiu hii inalenga kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti UKIMWI kitaifa na kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu zinazomaanisha maambukizi mapya sifuri, vifo vitokanavyo na UKIMWI sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo mwaka 2018”.
Kauli mbiu hii pia inahimiza utekelezaji wa dhati wa malengo ya Maendeleo ya Milenia na maazimio yaliyowekwa kwenye mkutano maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI uliofanyika mwaka 2001 nchini Marekani”, alisema Dkt. Mrisho.

Amesema kipaumbele cha maadhimisho ya mwaka huu ni upimaji wa hiari wa VVU na ushauri nasaha, na kutoa  wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapate huduma hii muhimu.

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wananchi kuadhimisha siku hiyo kwa njia ya makongamano, kumbukumbu za waliofariki kwa UKIMWI, midahalo, mikutano ya wazi, vipindi kupitia vyombo vya habari, kutembelea na kutoa misaada kwa watoto yatima na wanaougua ugonjwa huo  na kutoa elimu inayohusu kujikinga na maambukizi.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa TACAIDS Dkt. Raphael Kalinga amesema dawa hizo hutolewa  bila malipo kwa wahitaji wanaostahili kuzipata hii ni kulingana na mfumo wa utoaji kwa wahitaji.

“Kuna baadhi ya wagonjwa hulazimisha kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI ingawa kinga zao bado zinamudu kukabiliana na tatizo hilo wakati si sahihi kufanya hivyo. Kwani wanaostahili kupata dawa hizo ni wale ambao kinga zao zipo chini”, alisema  Dkt. Kalinga.

Maadhimisho ya wiki hiyo yataenda sambamba na maonyesho ya shughuli za wadau wa udhibiti UKIMWI nchini na kongamano la kitaifa la kutathimini hali  na mwelekeo wa udhibiti  wa ugonjwa huo. 

No comments:

Post a Comment