TANGAZO


Friday, November 21, 2014

Diamond Trust Bank Tanzania yafungua tawi la 21 mkoani Mtwara

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Diamond Trust Bank (DTB), Bw. Abdul Samji, akisaidiana kukata utepe na Meya wa Jiji la Mtwara, Mhe. Seleman Mtalika, wakati wakizindua tawi jipya la benki hiyo jijini Mtwara leo. DTB kwa sasa ina matawi 21 nchi nzima, na inapanga kufungua matawi mengine manne (4) mwaka 2015, kuongeza nguvu kwa mtandao wake kwa miji ya Mwanza na Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu, Novemba 21, 2014 
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Diamond Trust Bank Tanzania Limited (DTBT), Abdul Samji, amezindua tawi la Benki hiyo katika Manispaa ya Mtwara, lililopo katika Barabara ya Tanu, na hivyo kufanya Benki hiyo kuwa na matawi 21 nchini Tanzania.
Wakati Mwenyekiti Abdul Samji akizindua tawi la kwanza la DTB kwa Mikoa ya Kusini, alionyesha furaha yake kwamba kwa kipindi cha miaka 7 Diamond Trust Bank imefungua matawi mapya yapatayo 17 – wastani wa matawi 2 hadi 3 kwa mwaka. “Benki yetu ilianza na matawi 4 mwaka 2007 na leo ina matawi 21, huku tukiwa na mpango wa kufungua matawi mengine mawili ndani ya miezi mitatu ijayo,” alisema Samji huku akionesha uso wa furaha.
Akizungumza na wanahabari wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi wa tawi hilo, Samji amesema Benki yake imejizatiti na mpango wake wa kuendelea kufungua matawi nchini. “Kufunguliwa kwa Tawi la DTB katika Manispaa ya Mtwara ni utekelezaji wa hamu na shauku iliyo nayo benki yatu kuwa sehemu ya ukuzaji uchumi kwa mikoa ya kusini. DTB imekuwa ikitoa misaada ya kibenki kusaidia miradi kadhaa ya maendeleo na ya kimiundombinu ili kuwezesha kampuni zinazoendesha shughuli zao mkoani Mtwara. Tunaamini kuwapo kwa DTB Bank kwenye mkoa huu kutawarahisishia mambo mengi wateja wengi wapya watakaoanza kufanya nasi shughuli za kibenki.”
Sasa DTB inakuwa benki ya nane (8) ya kibiashara kufungua tawi katika Manispaa ya Mtwara huku ikitoa huduma kikamilifu za kibenki kwa wananchi wa Mtwara, na wakati huo huo ikiwa na mikakati ya kuelekeza nguvu zake kwa wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali. Samji amesema kwamba DTB imejizatiti katika kuunga mkono biashara ndogondogo ili  kuziwezesha kupata haraka mikopo itakayowafaa.

Akizungumzia mpango wao wa kuungana na Taasisi ya Aga Khan (Aga Khan Foundation-AKF) kuboresha mipango ya uchumi na fedha, kilimo, uboreshaji wa maisha ya wananchi, elimu na afya Kusini mwa Tanzania (kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi), Samji anasema: “Tumekuja Mtwara tukiwa na uhakika wa kazi nzuri iliyofanywa na Taasisi ya Aga Khan (AFK) miongoni mwa familia za wakulima wadogo wadogo katika Mikoa ya Kusini tukiwa tumejizatiti kuunga mkono juhudi zao hizo za pamoja. Tunatarajia kwamba kufunguliwa kwa Tawi la DTB la Mtwara, kutakuwa kama changamoto kwa programu ya maendeleo ya Taasisi ya Aga Khan ambayo imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi wengi waishio vijijini katika eneo hili.”
DTB inachukuliwa kuwa ni Benki inayokua kwa kasi kubwa sana nchini Tanzania; ikiwa na utendaji wa kiwango cha hali ya juu sana katika tasnia ya viwango vya kibenki. DTBT imeripotiwa kuwa na kiwango cha juu sana cha utendaji hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 30, 2014 ikiwa nyota katika ukuaji wa Faida Kabla ya Kukatwa Kodi (Profit Before Tax-PBT) ya 37.5% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2013. Faida kabla ya kodi ilifikia kiwango cha TZS 15.4 bilioni hadi robo ya tatu mwaka 2014 ikiwa na maongezeko ya kuvutia kutoka ukopeshaji na shughuli za fungani (treasury activities).
Mali za Benki zimeongezeka kwa TZS 128 bilioni kutoka TZS 505 bilioni mwezi Desemba 2013 hadi kufikia TZS 633 bilioni mwishoni mwa Septemba 2014, wakati mikopo kwa wateja (Net Advances to Customers) imeongezeka kwa TZS 62 bilioni.
DTB kwa sasa ina matawi 21 nchi nzima, matawi 8 yakiwa katika jiji la Dar es Salaam; mawili (2) jijini Arusha na tawi moja moja katika miji ya Zanzibar, Tanga, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Moshi, Morogoro, Iringa, Tabora, Kahama na ongezeko la tawi jipya la Mtwara. Benki inapanga kufungua matawi mengine manne (4) mwaka 2015, kuongeza nguvu kwa mtandao wake kwa miji ya Mwanza na Dar es Salaam huku kukiwa na uwezekano wa kupata matawi mapya kwa miji ya Singida na Kigoma katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Benki inaangalia kwa karibu uwezekano wa kupanua mtandao wake  maeneo ya Kusini mwa Tanzania katika miji ya Masasi, Lindi na Songea.

DTB Tanzania ni kampuni tanzu ya makampuni ya DTB (DTB Group) kiuhusiano na East African Bank, na kufanya shughuli za kibenki kibiashara na Kenya, Uganda na Burundi ikiwa na mtandao wa matawi 107 kwenye ukanda huu.
DTB ni kampuni tanzu ya Mfuko wa Aga Khan wa Maendeleo ya Kiuchumi (the Aga Khan Fund for Economic Development-AKFED), ambayo ni tawi la Mtandao wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (Aga Khan Development Network-AKDN).

No comments:

Post a Comment