TANGAZO


Friday, October 24, 2014

Waziri Ummy Mwalimu aitaka Halmashauri ya Kinondoni kusimamia Sheria za Mazingira

Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu, akizungumza na Watendaji wa Kata za Manispaa ya Kinondoni (hawapo pichani), wakati wa ziara yake kwenye manispaa hiyo jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mhandisi Mussa Natty.

Hussein Makame-MAELEZO
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu amewataka watendaji wa kata za halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za kusimamia mazingira kwani kufanya hivyo watafanikiwa katika kutunza mazingira ya halmashauri hiyo.
Naibu Waziri Mwalimu ameyasema hayo wakati alipofanya ziara katika Halmashauri ya Kinondoni jijini Dar es Salaam leo kujifunza jinsi halmashauri hiyo inavyosimamia taka zinazozalishwa katika maeneo yake.
Akizungumza mbele ya watendaji wa kata mbalimbali za halmashauri hiyo,alisema ni vyema wakajifunza kutoka halmashauri zilizofanikiwa katika kusimamia mazingira ambapo utekelezaji wa sheria zilizowekwa unafanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa.
“Iwapo mtasimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za kusimmamia mazingira  mlizozitunga itasaidia kutatatua changamoto za mazingira, naamini mtafanikiwa, hivyo naomba mkawe mabalozi kwenye kata zenu kusimamia mazingira” alisema Naibu Waziri Mwalimu.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha usimamizi wa mazingira unafanikiwa ni vyema halmashauri za jiji la Dar es Salaam zikaunganisha nguvu kwani suala la usimamizi wa mazingira linahitaji nguvu ya pamoja ili kulifanikisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashari ya Manispaa ya Kinondoni Mussa Natty alisema changamoto kubwa  inayowakabili ni vitendea kazi katika usafi wa mazingira ambazo zinakabiliwa na changamoto ya bajeti.
“Lakini pia kuna changamoto kuu mbili zinazotukabili, zipo zilizo nje ya uwezo wetu na nyingine zipo ndani ya uwezo wetu, changamoto iliyo nje ni ongezeko la idadi ya watu lililosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi-huwezi kuyazuia watu kuja mjini” alisema Natty.
 Aliongeza kuwa pamoja na kuliweka suala la mazingira katika sehemu ya shughuli za maendeleo, lakini pia wana mpango wa kununua mashine kwa ajili ya kusafisha mifereji ya Kinondoni ili kuepuka mafuriko yanayotokea wakati wa mvua.
“Hata hivyo, bado kwenye taka ngumu tuko nyuma lakini tunategemea kupata msaada kutoka kwa Wajerumani kupitia jiji la Hamburg watatusaidia fedha tumesaini nao mkataba atakuja rais wa senate ya jiji kushughulikia suala hilo”
Alisema fedha zinazotarajiwa kutolewa ni karibu fedha za Ulaya EURO milioni 1.5, ambazo wanaamini zitasaidia katika kufanikisha sualala usimamizi wa mazingira katika halmashauri hiyo.
Alisema kwa siku halmashauri ya Kinondoni inazalisha taka tani 206 wakati ni aslimia 62 tu ndio zinazokusanywa huku akieleza lengo kuwa ni kukusanya taka zote zinazozalishwa na kwa sasa kila jumamosi ya kwanza ya mwezi ni siku ya usafi wa mazingira.
Mbali na kuzungumza na watendaji na uongozi wa halmashauri hiyo, Naibu Waziri Mwalimu alitembelea baadhi ya masoko ya Kinondoni ikiwemo soko la TANDALE na halmashauri ya wilaya ya Temeke ili kujifunza changamoto za mazingira.
Wakati akitembelea soko la Tandale Naibu Waziri Mwalimu, alielezwa changamoto mbalimbali zinazolikabili soko hilo huku suala la ukosefu wa vitendea kazi likchukua nafasi kubwa.
Akieleza masuala mbambali ya soko hilo, Mwenyekiti wa soko hilo Sultan Kiumbo alisema kwamba mbali na changamoto hiyo suala la miundombinu ya soko ni changamoto katika kusimamia mazingira.
Hivyo, aliiomba halmashauri ya Kinondoni kuziangalia changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi ambapo Afisa Usafishaji wa Halmashauri hiyo Rajabu Ngoda aliahidi kupeleka gari la kuzoa taka kila siku ili kufanikisha usimamizi wa mazingira ya soko hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri Mwalimu aliutaka uongozi wa soko hilo kujenga utaratibu wa kutoza adhabu wafanyabiashara na wananchi wanaotupa taka kwani hiyo ni njia itakayosaidia watu kuacha kufanya hivyo.
Aliongeza kusema kuwa Serikali inalishughulikia suala la mifuko midogo ya plastiki inayotumiwa na wafanyabiashara lakini aliwataka wafanyabiashara kuiungana mkono Serikali kwa kuuuza mifuo hiyo ili kupunguza matumizi yake.

No comments:

Post a Comment