TANGAZO


Thursday, October 16, 2014

Serikali ya Tanzania yapokea zaidi ya Sh. Bilioni 10

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Doroth Mwanyika (kushoto) akitia saini mkataba wa ushirikiano wa Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM)  Awamu ya IV kwa niaba ya Serikali ya Tanzania leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Doroth Mwanyika (kushoto) akibadilishana hati ya mkataba wa ushirikiano wa Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) Awamu ya IV waliosaini leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Doroth Mwanyika (kushoto) akishukuru Serikali ya Finland kwa ushirikiano mzuri wanaoendelea kuipa Tanzania mpaka sasa na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika katika malengo yaliyokusudiwa. Kulia ni Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila.
Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila  (kulia)PFM akiongea na waandishi wa habari  (hawapo pichani) na kuipongeza kwa kusimamia fedha za umma na kuwa na uongozi unaosimamia utawala wa kidemokrasia, uchumi imara, ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo na hivyo kupunguza umasikini. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dae es salaam wakati wa kusaini mkataba wa ushirikiano wa Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM)  Awamu ya IV. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Doroth Mwanyika.
Baadhi ya waandishi wa habari  waliohudhuria hafla ya kusaini mkataba wa ushirikiano wa Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM)  Awamu ya IV kati ya Serikali ya Tanzania na Finland leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Eleuteri Mangi- MAELEZO)

Na Eleuteri Mangi -MAELEZO
16/10/2014
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea Sh. Bilioni 10.1 ambazo ni sawa na EURO milioni 4.8 kutika Serilkali ya Finland ikiwa kwa lengo la ushirikiano wa Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM)  Awamu ya IV.
Mkataba wa makubaliano hayo umesainiwa leo jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Doroth Mwanyika kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila.
Bi. Doroth amesema kuwa Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma Awamu ya nne ametanguliwa na Awamu ya I hadi III ambapo awamu hizo zimeonesha mafanikio mbalimbali nchini.
Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa mapato kutoka Sh. Bilioni 390 mwaka 2009/2010 hadi zaidi ya Sh. Bilioni 700 kwa mwezi mwaka 2013/2014 na kuboresha mifumo ya kifedha kwa kutumia mifumo ya kielektroniki kwa kulipa moja kwa moja kwenye akaunti husika.
Bi Doroth metaja mafanikio mengine kuwa ni ubureshwaji wa utendaji watumishi wanaosimamia masuala ya mpango wa PFM kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) na utendaji kazi mzuri wa kamati za Bunge zinazohusika na ufuatiliaji wa matumizi ya Fedha za umma.

Aidha, Bi. Doroth ameishukuru Serikali ya Finland kwa ushirikiano mzuri wanaoendelea kuipa Tanzania na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika katika malengo yaliyokusudiwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kupunguza umasikini nchini.

Naye Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila amesema kuwa usimamizi mzuri wa fedha za umma (PFM) umeifanya nchi yake kuongeza fedha kwa ajili ya mpango huo.

“PFM ni muhimu kwa utawala wa kidemokrasia, uchumi imara, ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo na hivyo kupunguza umasikini” alisema Bi. Sanikka.

Ufanisi wa usimamizi mzuri wa fedha za umma umewezesha ufanisi wa malighafi zilizopo nchini katika kuboresha elimu, kutoa huduma bora za kiafya, kuongeza mazao ya kilimo na kuendeleza utalii.

Mpango wa PFM upo katika awamu ya nne na ulianza 2012 na unatarajiwa kuishia 2017 ambapo awamu ya I hadi III ilianza 1998 na kumalizika 2012, Finland imekuwa nchi ya sita mhisani katika kusaidia mpango huu wa mageuzi.
Nchi nyingine wahisani ni pamoja na Canada, Ujerumani Ireland na Uingereza.  


No comments:

Post a Comment