Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeshutumu kwamba kikundi cha Somalia cha wapiganaji wa Al Shabaab bado kinaendelea na biashara ya mkaa katika bandari ya Kismayo, licha ya biashara hiyo kupigwa marufuku na Umoja wa Mataifa mwaka 2012.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa magunia milioni moja yanasafirishwa nje ya Somalia yakishuhudiwa na jeshi la Kenya ambalo lipo katika bandari hiyo.
Awali serikali ya Kenya ilikanusha kuhusika kwa namna yoyote na biashara hiyo ya mkaa.
Ripoti hiyo inasema kikundi cha wapiganaji wa Al Shabaab wa Somalia, jeshi la Kenya na utawala wa Kismayu wote wananufaika na biashara ya mkaa.
Al Shabaab wanasemekana kusafirisha mkaa katika kiwango kikubwa kutoka bandari ya Kismayu kwenda katika nchi za ghuba ya Uajaemi na kutokana na biashara hiyo walipata dola za Kimarekani milioni $250t kati ya mwaka 2013 na 2014.
Kikundi cha Umoja wa Mataifa, ambacho kilichunguza suala hilo, wamesema katika uchunguzi wao walitumia picha za satelaiti kukusanya ushahidi na taarifa kutoka vyambo vya habari vya eneo hilo.
Al Shabaab wameendelea kunufaika na mapato yanayokusanywa ambayo ni makubwa kuliko wakati kikundi hicho kilipokuwa kikidhibiti bandari ya Kismayu, biashara yote hiyo imekuwa haibughudhiwi na mashambulio ya kijeshi dhidi ya kikundi hicho.
Operesheni katika bandari hiyo zinasimamiwa kwa pamoja na wanamgambo wa Ras Kamboni, jeshi la eneo hilo ambalo ni sehemu ya utawala wa muda wa Jubaland.
Umoja wa Mataifa ulipiga marufuku usafirishaji wa mkaa kutoka Somalia mwezi Februari 2012 katika jitihada za kupunguza vyanzo vya mapato kwa kikundi cha Al Shabaab.
No comments:
Post a Comment