Na Aron Msigwa –MAELEZO.
11/9/2014. Dar es salaam.
HATUA iliyochukuliwa na
uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kuendelea kuweka
msisitizo katika usimamizi wa maadili kwa wanafunzi imeanza kuzaa matunda
kufuatia kuogezeka kwa ufaulu wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.
Hayo yamebainishwa leo
jijini Dar es salaam na mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE)
Prof. Emanuel Mjema wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho
yanayoendelea ya chuo hicho kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake Januari,
1965.
Amesema suala la usimamizi
wa maadili kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia chuoni hapo limepewa
kipaumbele kikubwa na uongozi wake tofauti na miaka iliyopita hali ilinayokifanya
chuo hicho kuwa mfano wa kuigwa vyuo pamoja na taasisi nyingine za elimu ya juu
hapa nchini.
“Chuo chetu sasa ni
mfano wa kuigwa na vyuo vingine hapa nchini kwa sababu tumeweza kusimamia suala
la maadili hasa uzingatiaji wa mavazi yenye staha kwa wanafunzi hali
iliyoongeza heshima kwa chuo chetu”.
Mbali na suala la usimamizi
wa mavazi kwa wanafunzi Prof amesema chuo hicho kimeendelea kuhakikisha ulinzi
na usalama kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia na kutoka katika mazingira
ya chuo hicho, kuimarisha ukaguzi katika maeneo yote muhimu ya kuingilia
wanafunzi na kuwatambua wanafunzi wote kwa kutumia vitambulisho vyao.
Amefafanua kuwa chuo
hicho sasa kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake yakiwemo mabadiliko na maboresho makubwa
katika sekta ya elimu hasa ongezeko la
udahili wa wanafunzi, ongezeko la fani za masomo na kampasi za chuo hicho
katika mikoa mingine nchini ikiwemo Dodoma, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.
Prof. Mjema amefafanua
kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50 kikiwa chuo pekee Afrika ya
Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.
“Chuo hiki pekee ndicho
kinachotoa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya vipimo, ni chuo kinachotegemewa sana
katika ukanda huu wa nchi za Afrika Mashariki na SADC” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa tangu
kuanzishwa kwake Januari, 1965 na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere , chuo hicho kimepata
mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka
kutoka wanafunzi 25 mwaka 1965 hadi 14,000 mwaka 2014.
Mafanikio mengine ni
kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia shahada,
kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD) chuoni hapo pamoja na chuo kuanzisha ushirikiano wa elimu
na vyuo vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland
katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi
za SADC.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 50 ya chuo hicho idadi ya
kampasi imeongezeka kutoka 1 ya jijini Dar es salaam na kufikia 4 katika mikoa
ya Mbeya, Mwanza, Dodoma na upande wa Zanzibar huku idadi ya wahitimu wa chuo
hicho ikiongezeka kwa kipindi chote ikiwa zaidi ya wanafunzi Laki moja.
Aidha, katika
kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kwa
wanafunzi katika maadhimisho hayo,chuo kinaandaa matukio mbalimbali ya ukusanyaji
wa fedha kupitia chakula cha hisani, matembezi, midahalo ya wasomi na mikutano
wanafunzi wahitimu wa chuo hicho Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Dar es
salaam kwa ajili ya ujenzi wa maabara, vyumba vya mihadhara ya wanafunzi
na madarasa.
Pia chuo hicho
kinaandaa mafunzo ya ujasiriamali yatakayotolewa kwa jamii ikiwa ni sehemu ya
kurudisha huduma kwa jamii kwa kuwajengea uwezo
wajasiriamali, na kuwajengea uelewa wanafunzi ili waweze kuwa na
uchaguzi sahihi wa hatima yao ya baadaye pindi wanapohitimu mafunzo.
No comments:
Post a Comment