TANGAZO


Wednesday, September 10, 2014

Profesa Mwandosya ataka suala la rushwa kuingizwa katika Katiba Mpya


 Profesa Mark Mwandosya

Na Magreth Kinabo, Dodoma
10/09/2014
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Profesa Mark Mwandosya amependekeza kwamba suala la rushwa litambuliwe katika Katiba Mpya, inayopendekezwa ili kuweza kuongeza nguvu ya kupambana nalo.
 
Kauli hiyo imetolewa  leo na Mwandosya, ambaye pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum) wakati akichangia mjadala wa kujadili sura zilizobakia za Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kikao cha thelasini  na saba cha Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, ambacho kinaendelea  na sura ya Pili, Tatu, Nne na Tano za Rasimu hiyo.
Mhe. Mwandosya alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akichangia sura ya Tatu  kuhusu Maadili ,Miiko  ya Uongozi na Utumishi wa Umma.
“ Lazima  suala la rushwa litambuliwe katika Katiba hii.Serikali zote mbili zitatunga sheria ili tuweze sasa kupigana na adui rushwa. Ni suala la kwetu sote halina muungano, lazima litambuliwe vinginevyo  hii vita tutashindwa,” alisisitiza Mhe. Mwandosya.
Akizungumzia kuhusu suala la rushwa mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Mhe. Dkt. Mary Mwanjwela akichangia sura hiyo alisema rushwa ni adui wa haki dunia nzima na Tanzania inaelewa pia ni sehemu ya utawala bora.
“Hili ni jambo linalorudisha maendeleo nyuma.Mimi ninawaomba wajumbe wenzangu tuliingize katika Katiba tusipoliingiza tutakuwa hatueleweki,” alisema Dkt. Mwanjwela. 

Aidha Mhe. Mwandosya alisisitiza katika sura ya pili   kupata bidhaa na huduma bora zenye viwango ni jambo muhimu.
 Aliongeza kuwa kiuchumi Serikali itachukua hatua zinazofaa… ili kuwezesha ushindani wenye hali ya tija.
“ Regulation   liwe kwenye Katiba itakuwa ni mapinduzi… si suala la Serikali bali la vyombo maalum,” alisema.
Profesa Mwandosya akichangia kuhusu sura ya Nne inayohusu Haki za Binadamu alisema mazingira safi ni suala mtambuka ni vema kuwa katika Katiba, kila Mtanzania kupata maji safi na salama, hivyo Katiba inaweza kusema  kwani ni jambo la kitaifa ambalo litafanikiwa kwa kuwa ni wajibu wa Serikali , lakini si kwa kuipeleka mahakamani.
Alizungumzia pia kuhusu nyumba na makazi bora ni haki ya binadamu  inaendana  na mazingira safi na salama, hivyo likiwekwa katika Katiba  ni lazima kila Mtanzania ataishi katika mazingira safi na salama.

No comments:

Post a Comment