Waziri wanchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Hawa Ghasia (MB).
· Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Mhe. Dkt. Kebwe Steven Kebwe (MB)
· Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Joel
Bendera
· Mstahiki Meya wa Manispaa Morogoro Mhe.
Amiri Nondo
· Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Charles Pallangyo
·
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa – Ndg. Noel
Kazimoto
·
Naibu Katibu Mkuu – OWM-TAMISEMI, Dkt.
Deo Mtasiwa
·
Kamishina, Idara ya Ustawi wa Jamii,
Ndg. Dunford Makala
·
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani
(WHO), Dkt. Rufaro Chatora
·
Wakurugenzi wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii na OWM - TAMISEMI,
·
Waganga Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara,
·
Waganga Wakuu wa Wilaya Tanzania Bara
·
Maafisa Waandamizi wa Serikali na
Mashirika yasiyo ya Kiserikali,
·
Wadau wote wa Sekta ya Afya,
·
Waandishi wa Habari,
·
Wageni Waalikwa,
·
Mabibi na Mabwana.
Awali
ya yote naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya
njema inayotuwezesha kukutana hapa leo.
Naelewa kwamba ninyi nyote mmeacha majukumu mengi yenye umuhimu ili
muweze kushiriki katika mkutano huu ambao unalenga kuboresha huduma za afya na
ustawi wa jamii nchini kote. Kama
mlivyoelezwa katika barua za mwaliko, Mkutano huu ni sehemu ya kazi zetu, hivyo
basi ni tegemeo langu kuwa kila mmoja wetu atashiriki kikamilifu katika
majadiliano, ili hatimaye sisi sote tukubaliane nini kifanyike katika kuboresha
huduma, hususan jinsi ya kushughulikia changamoto zinazotukabili katika kutoa
huduma za afya na ustawi wa jamii.
Katika
ziara nilizofanya sehemu mbalimbali hapa nchini nimeshuhudia juhudi
zinazofanywa na wadau katika kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya
na ustawi wa jamii. Baadhi ya juhudi hizo ni pamoja na kujenga vituo vipya vya
huduma za afya, kukarabatiwa vile ambavyo havipo katika hali nzuri, kuongeza
watumishi na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, kuimarisha utaratibu wa
kukusanya mapato katika vituo, utoaji wa huduma kwa makundi maalum
hususan,wanawake wajawazito,watoto chini ya miaka mitano na wazee katika baadhi
ya maeneo husika.Aidha, malalamiko kuhusu uhaba wa dawa na vitendo vya rushwa
yamepungua katika maeneo ambayo kumefanyika juhudi hizo.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Nafarijika
kuona kuwa baadhi yenu mmeanza kuchukua hatua za kuboresha hali ya miundombinu ya
vituo vya huduma za afya. Hizi ni
jitihada zinazotakiwa kupongezwa kwani, ndiyo utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM). Ni
dhahiri kuwa uboreshaji huu unahitaji fedha.
Sote tunaelewa kuwa, fedha kutoka Serikalini peke yake hazitoshi
kutuwezesha kutekeleza yale tunayopanga.
Hivyo basi ni wazi kuwa lazima kuwepo na jitihada za kupata fedha kutoka
vyanzo vingine ili zisaidie kutekeleza kazi zinazopangwa. Nimefarijika kusikia kuwa tayari baadhi yenu
mmeonesha kuwa inawezekana kabisa kuboresha kwa kiwango kikubwa makusanyo ya
fedha kutoka vyanzo vilivyopo, hususan Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF). Hii inanipa matumaini kuwa
inawezekana kuboresha makusanyo kutoka vyanzo vingine ikiwa ni pamoja na Mfuko
wa Afya ya Jamii (CHF na TIKA) na uchangiaji wa papo kwa papo (User fees).
Hivyo basi, niendelee kutoa rai kwenu nyote muendelee kuweka msisitizo katika
makusanyo kutoka katika vyanzo hivyo.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Ni
matumaini yangu kuwa katika Mkutano huu tutajifunza jinsi wenzetu walivyofanya
hadi wakafikia mafanikio mazuri waliyopata.
Kwa taarifa tulizonazo vituo vyote vilivyoonesha mafanikio, vimeongeza
makusanyo zaidi ya mara tatu, kutoka kiwango kilichokuwepo kabla ya kuchukua
hatua za kuboresha makusanyo. Habari
njema katika mafanikio waliyopata ni kwamba hakukuwa na ongezeko la gharama za
huduma zinazotolewa kwa wagonjwa/wateja katika vituo husika. Naamini uongozi wa vituo hivyo ulitafakari na
kuainisha changamoto zilizokuwa zikichangia katika hali iliyokuwepo na kisha
kuchukua hatua za kushughulikia changamoto hizo. Ni dhahiri kuwa kila mmoja wenu anaweza
kuchukua hatua hizo na kupata mafanikio hayo.
Kwa mafanikio yaliyooneshwa na wale waliojituma, tumekubaliana kuwa
Kauli Mbiu ya Mkutano wa mwaka huu iwe: “Kuongeza mapato katika vituo vya
huduma za afya vya umma bila kuongeza gharama za huduma inawezekana. Kila mdau atimize wajibu wake”.
Naelewa
kuwa kuna changamoto nyingi katika kuongeza mapato zinazovikabili vituo vya
huduma za afya vya umma katika ngazi zote.
Changamoto ya msingi ambayo naamini inavikabili vituo vingi vya umma,ni
ukusanyaji wafedha zinazotokana na kuhudumia wagonjwa kama inavyotakiwa na
kuziwasilisha kunakohusika, hususan zile zinazotokana namalipo ya papo kwa papo
na kutozingatia taratibu za kuandaa madai baada ya kuhudumia wanachama wa
Mifuko ya Afya, ikiwemo; Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mfuko wa Afya ya Jamii
na mingineyo.Hii inawezekana kuwa inasababishwa na wahusika wa ukusanyaji wa
mapato hayo kutowajibika ipasavyo, kutokuwa na elimu ya kutosha hasa, uandaaji
wa madai na ufuatiliaji wa malipo. Vile
vile, kukosekana kwa motisha kwa watumishi hao kunaweza kuchangia katika hali
hiyo. Naamini vituo vyote
vilivyofanikiwa katika eneo hili vimezikabili changamoto hizo na kupata
mafanikio hayo.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Nimefarijika
sana kuwa Mkutano huu utafuatiwa na Mkutano mwingine wenye lengo la kujadili
pitio la Mwongozo wa uchangiaji wa gharama za huduma za afya. Mafanikio yaliyopatikana yanahusu ukusanyaji
wa fedha zinazotokana na huduma zinazotolewa kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya. Uchangiaji wa papo kwa
papo nao ukiwekewa mazingira mazuri unaweza kuwa chanzo kingine kikubwa cha
mapato katika hospitali au kituo chochote kinachotoa huduma za afya. Natumaini kwamba pamoja na mambo mengine
muhimu mtajadili udhibiti katika kukusanya, utunzaji na matumizi ya fedha
zinazokusanywa, kwani hizo ni fedha taslimu na kama hakutakuwa na usimamizi
unaotakiwa, tutaendelea kwa na tofauti kubwa kati ya fedha zilizokusanywa na fedha
zilizoandikwa katika vitabu. Hali hiyo,
itawapa mwanya watu wachache wenye nia mbaya kuendelea kunufaika wakati
wananchi wanaendelea kukosa huduma.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Mkutano
wa mwaka jana 2013, ulitudhihirishia kuwa usimamizi elekezi ukifanywa vizuri
ndiyo msingi wa utoaji wa huduma bora.
Nategemea kuwa katika Mkutano huu suala hili litasisitizwa zaidi. Bila usimamizi mafanikio yatakayopatikana
hayatakuwa endelevu. Mengi katika hayo
yatabaki kuwa ni historia tu kwamba mwaka fulani tulifanikiwa kuinua mapato kwa
asilimia 300, lakini baada ya mwaka moja tu mapato yalishuka. Naomba tuelewe kuwa katika kila fanikio mara
nyingi changamoto hazikosekani.
Changamoto hizi zinaweza kusababishwa na baadhi ya watu waliokuwa
wananufaika kwa kujichukulia sehemu ya makusanyo kinyume na utaratibu. Kuboresha usimamizi wa makusanyo ina maana ya
kuziba mianya ya ubadhirifu wao, hivyo nidhahiri watafanya kila juhudi kuhujumu
mafanikio hayo. Lazima tuwe macho na
watu wa aina hii. Kuna mifano hai katika
sehemu mbalimbali ambapo usimamizi wa makusanyo uliimarishwa na watu hao
wakajaribu kuhujumu jitihada hizo.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Kufanikiwa
katika kushughulikia changamoto zinazoainishwa, katika suala lolote kunachangia
kwa kiasi kikubwa katika mafanikio yanayopatikana baadaye. Kutoshughulikia changamoto kadiri
zinavyojitokeza, kunasababisha kuongezeka kwa changamoto hizo na hivyo kuathiri
utoaji wa huduma, ziwe za afya au ustawi wa jamii. Nadiriki kusema kuwa malalamiko mengi
yanayotolewa kuhusiana na huduma tunazotoa yanatokana na kutoshughulikia
changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na kuachwa bila kushughulikiwa
ipasavyo. Nawakumbusha kuwa, jukumu la
kwanza kwa kituo chochote cha huduma za afya au ustawi wa jamii ni kutoa huduma
zenye ubora unaotakiwa na kwa gharama nafuu.
Naamini kuwa katika mada zitakazowasilishwa katika mkutano huu suala
hili litajadiliwa na mifano hai itatolewa nawale walioonesha mfano wa kuigwa
katika kutekeleza majukumu yao.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Katika
Mkutano wa mwaka jana tuliona jinsi uwajibikaji wa viongozi ulivyoboresha hali
ya upatikanaji wa dawa za kutosha kwa wakati wote, katika vituo kadhaa vya umma
katika maeneo yao ya kazi. Haya yalikuwa
ni matokea ya viongozi wa sekta ya afya walioamua kutekeleza majukumu yao kwa
ufanisi kama inavyoelekezwa katika sera, miongozo na kanuni za kazi. Viongozi hawa walionesha mfano mzuri. Wapo viongozi ambao kwa sababu wanazoelewa
wao waliamua kutotekeleza majukumu yao kikamilifu. Katika Hotuba ya kufunga Mkutano wa mwaka
jana, ilani ilitolewa kwa viongozi watakaofanya vibaya bila kuwa na sababu za
msingi, kwamba watashughulikiwa kulingana na taratibu zilizopo. Ni matumaini yangu kuwa katika Mkutano huu,
tutaelezwa kuwa idadi ya waliofanya vyema imeongezeka baada ya wahusika
kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinavyotakiwa
vinapatikana katika vituo wakati wote.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Mwaka
huu kumekuwa na matukio ya hapa nchini na nje ya nchi yaliyotufanya tuongeze
zaidi kiwango cha tahadhari. Kwanza
kulitokea mlipuko wa ugonjwa wa Dengue, ambao uliwapata wagonjwa 1384 kote
nchini, sehemu kubwa ya wagonjwa hao walikuwa ni wa Dar es Salaam (86%). Ugonjwa huu ulisababisha vifo vya watu 4,
hapa Dar es Salaam. Tukio la pili ni
ugonjwa wa Ebola, ambao kwanza ulianzia nchi za Afrika Magharibi. Kuanzia katikati ya mwezi Machi hadi Agosti,
2024 watu 3069 waliugua ugonjwa huu na hadi kufikia tarehe 28 Agosti, 2014
ugonjwa huu umeua watu 1552 . Hivi
karibuni ugonjwa huu umeingia nchi ya Congo DRC. Hadi mwishoni mwa Mwezi Agosti watu 24
wameripotiwa kuugua ugonjwa huu.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Hapa
nchini ugonjwa wa Ebola haujathibitika kuingia.
Hata hivyo Serikali imechukua tahadhari zote kuhakikisha kuwa ugonjwa
huu hauingii hapa nchi na kama ukiingia, “Mwenyezi Mungu apishilie mbali”
utadhibitiwa kikamilifu. Ni matumaini
yangu kuwa katika Mkutano huu, suala la magonjwa ya mlipo kama haya
yatajadiliwa kikamilifu ili kila mmoja wetu awe katika tahadhari kubwa.
Napenda
kutumia fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa Watu wa Marekani kupitia Shirika
lao la CDC na Shirika la Afya Duniani kwa kutoa vifaa na vifaa tiba kwa ajili
ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.
Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wote waliojituma katika
kushughulikia magonjwa haya. Najua kuwa
walikuwa wanahatarisha afya zao na hata maisha yao hasa pale ilipoonekana kuwa
huenda tayari ugonjwa wa Ebola umeingia nchini kupitia kiwanja cha ndege cha
Mwalimu Julius Nyerere. Nawaomba ninyi
nyote muendelee na juhudi hizo ili ugonjwa wa Ebola usiingie hapa nchini, kwani
ikitokea hivyo tutakuwa na wakati mgumu wa kuudhibiti, hasa ukizingatia
misongamano inayotokea katika vyombo vya usafiri, mila na desturi ambazo
zitachangia sana katika kuenea kwa ugonjwa huu kwa haraka.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Naomba
kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirika la Afya Duniani kwa
mchango wake mkubwa uliowezesha Mkutano huu kufanyika. Naamini utendaji wetu kwa ujumla umekuwa
chachu katika kulifanya shirika hili kuona umuhimu wa kuendelea kufadhili
Mkutano huu muhimu. Aidha, napenda
kuishukuru Benki ya Dunia kwakuchangia katika kufadhili Mkutano utakaoendelea
baada ya huu, kwa sababu Mkutano huo utaendeleza masuala ya kuboresha
upatikanaji fedha katika vituo vya huduna za afya kutokana na vyanzo vyao. Napenda kuwaahidi kuwa serikali itaendelea
kuthamini michango yao katika kuboresha upatikanaji wa huduma na kuziboresha
ili ziwafikie wananchi wengi zaidi na hatimaye wananchi wote waweze kupata
huduma bora, kwa gharama nafuu na kuzipata karibu na makazi yao. Ni mategemeo yangu kuwa wadau wengine wataiga
mfano uliooneshwa na Mashirika haya.
Ndugu
Wajumbe wa Mkutano,
Baada
ya kusema haya sasa napenda kutamka kuwa, Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na
Halmashauri wa mwaka 2014 umefunguliwa rasmi.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment