Spika wa Bunge
la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Dkt. Magreth Zziwa (wa pili kulia), akipewa
maelezo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TICS, Paul Wallace namna kampuni yake
inavyofanya kazi ya kupakua na kupakia mizigo katika bandari ya Dar es Salaam,
wakati wa ziara ya Wabunge wa bunge hilo, walipotembelea Ofisi za Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA), leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Eleuteri
Mangi-MAELEZO)
Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wakitembelea Bandari ya Dar es Salaam, walipofika Ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) leo jijini.
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
Jumuiya ya Afrika
Mashariki iko makini katika kutekeleza majukumu yake na iko karibu na watu wake
kwa kuwahudumia kupitia nchi washirika.
Kauli hiyo imetolewa na
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Dkt. Magret Zziwa wakati
wa ziara yake alipotembelea ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja
na wabunge wa bunge hilo leo jijini Dar es salaam.
Spika Dkt. Zziwa
alibainisha kuwa lengo la ziara ya wabunge hao ni kujionea shughuli mbalimbali
zinazofanywa na TPA na Bandari ya Dar es salaam kwa ujumla katika kuhudumia
nchi washirka kiuchumi na kujiamii.
“Ni muhimu kuifanya
Jumuiya kuwa imara zaidi kiuchumi na kijamii ili kuwahudumia watu wetu kwa
umahiri na umakini mkubwa katika mahitaji yao” alisema Spika Dkt. Zziwa.
Wabunge hao walitembelea
maeneo mbalimbali bandarini hapo na kujionea shughuli zinazofanywa ikiwa ni
pamoja na kupakia na kupakua mizigo inapoingia au kutoka ili kusafirishwa
kwenda nchi husika.
Spika Dkt. Zziwa
alisisitiza kuwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanahitaji kuona
jumuiya yao inavyowajali na kuwahudumia wanapotekeleza majukumu yao
ikizingatiwa kuwa kwa sasa hakutakuwa na urasimu wa kusafirisha mizigo kutoka
nchi moja kenda nyingine kwa kukaguliwa
mara mbili ambapo kwa sasa utaratibu wa Himaya Moja ya Forodha umeanza
kutekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Akionesha umuhimu wa
uchukuzi na usafirishaji wa mizigo kati ya nchi washirika, Naibu Waziri wa
Wizara ya Ushirikiano ya Afrika Mashariki, Dkt. Abdala Juma Abdulla Saadalla
amefananisha bandari, reli na barabara katika nchi kuwa ni sawa na “moyo na
mishipa ya damu” ambapo amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea
kuboresha reli zilizopo ili ziweze kutoa huduma kwa wakati.
“Tayari Serikali
kupitia wataalamu wake wa ndani imeboresha vichwa vya treni nane hadi sasa
ambapo vinatarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani pamoja na makasha” alisema Naibu
Waziri Saadalla.
Kwa upange wake Meneja
wa Bandari ya Da es salaam Awadh Massawe alipokuwa akiwaeleza Wabunge wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki namna TPA inavyofanya kazi, amesema kuwa kwa mwaka
2013/2014 mizigo inayosafirishwa kutoka bandarini hapo imeongezeka kutoka tani
milioni 4.05 mwaka 2012/13 hadi tani milioni 4.45 mwaka 2013/2014 ambayo ni
sawa na asilimia 9.8.
Massawe amesema kuwa
mizigo hiyo ilisafirishwa kutoka bandari ya Dar es salaam kwenda nchi za
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Burundi, Rwanda, Malawi and Uganda kwa
kutumia mifumo ya barabara na reli.
Massawe amesema kuwa
bandari ya Dar es salaam imekuwa ni kiunganishi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa kutumia mitandao iliyopo ya njia ya reli na barabara.
Kwa upande wa reli, Massawe
amesema kuwa Bandari ya Dar es salaam inaunganishwa na reli ya kati kwenda
Mwanza na Kigoma hali inayorahisisha nchi za Burundi, Rwanda na Kongo DRC
kufikika kirahisi na TARZARA ambayo inakwenda hadi Zambia.
Kwa njia ya barabara, Bandari ya Dar es
salaam inaunganisha Tanzania na nchi nyingine
kuanzia Dar es salaam kupitia Dodoma/Isaka/Rusumo
/Kabanga, Kigali hadi Bujumbura kwa Rwanda na Burundi, vilevile
Dodoma/Mwanza/Mutukula hadi Kampala Uganda.
Aidha, Massawe amesema
kuwa kwa mwaka 2013/2014 kumekuwa na jumla ya asilimia 30.4 ya mizigo yote
ilihudumiwa na bandari ya Dar es salaam.
Massawe amesema kuwa ongezeko
hilo la usafirishaji wa mizigo linatokana na maboresho yaliyofanywa bandarini
hapo kuhusu namna ya usafirishaji wa mizingo kufuatia mfumo wa Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuboreshwa kwa taratibu za kibiashara nchini na nchi
inapopelekwa mizigo hiyo.
Naye Kaimu Kamishina wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Lusekelo Mwaseba alifafanua faida ya mfumo wa Himaya Moja ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa unatarajiwa kupunguza gharama za
kufanya biashara na kuondoa urasimu wakati wa usafirishaji mizigo, kupunguza
gharama za kiutawala, kuondoa uwezekano wa rushwa na kuimarisha matumizi ya
mifumo ya mawasiliano (ICT) taktika kubadilishana taarifa miongoni mwa nchi
washirika.
Ziara hiyo ilijumuisha
Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makamishina kutoka Burundi,
Rwanda, Kenya, Uganda, mwenyeji Tanzania pamoja na Viongozi na watumishi wa TPA.
No comments:
Post a Comment