TANGAZO


Saturday, August 30, 2014

NECTA yafumua mfumo wa ufaulu kwa mitihani ya kidato cha nne na cha sita

*Matokeo ya ufaulu sasa hayatabadilika
*Watakaofanya vibaya hawana pa kuponea

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde.

Na Mwandishi wetu
BARAZA la Mitihani la Tanzania(NECT), limetangaza  mfumo mpya wa upangaji ufaulu kwa mitihani ya kidato cha nne na cha sita ambao sasa watatumia mfumo wa wastani wa pointi.
Kwa mujibu wa baraza hilo ni kwamba mfumo huo wa wastani wa pointi hautakuwa wa kubadilika ambao ni tofauti na ule uliokuwa unatumjiwa awali ambapo viwango vya ufaulu vinaweza kubadilika.
Akitangaza mfumo huo Dar es Salaam leo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema katika mfumo wa viwango vya ufaulu visivyobadilika ,viwango vya ufaulu vinavyofanana hupangwa ili viwe kipimo cha ufaulu kwa masomo yote kila mwaka.
“Kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 2011 Baraza la Mitihani lilikuwa likitumia mfumo wa viwango vya ufaulu vinavyobadilika.
“Hata hivyo kwa kuzingatia maoni ya wadau wa elimu kuanzia mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 ,baraza liliamua kutumia mfumo wa viwango vya ufaulu visivyobadilika,”alisema Dk.Msonde.
Alifafanua ili kupata viwango vya ufaulu visivyobadilika ,baraza lilizingatia wastani wa viwango vya ufaulu vilivyotumika kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2011.
Alisema baraza lililenga kupunguza mlundikano wa alama na  kuwianisha viwango vya alama za mitihani ya kidato cha nne (CSEE) na mtihani wa kidato cha Sita (ACSEE).
Pamoja na hayo alisema ipo mifumo anuwai inayotumiwa na nchi mbalimbali duniani katika kupanga viwango vya ufaulu vinavyobadilika na mfumo wa viwango visivyobadilika.
Alisema katika mfumo wa viwango vinavyobadilika ,viwango vya ufaulu hupangwa kwa kutegemea jinsi watahiniwa walivyofaulu somo husika. 
Katika mfumo wa ufaulu usiobadilika , viwango vya ufaulu vinavyofanana hupangwa ili viwe kipimo cha ufaulu kwa masomo yote kila mwaka.
Dk.Msonde alifafanua mifumo inayotumika kupanga madaraja ya ufaulu ni mfumo wa jumla ya pointi na mfumo wa wastani wa pointi.
Alisema mfumo wa jumla ya pointi ni mfumo ambao madaraja ya ufaulu hupangwa kwa kutumia jumla ya pointi .Mfumo huo umekuwa ukitumika kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 2014 kulingana na muongozo wa matumizi ya viwango vya ufaulu na utaratibu wa kutunuku matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na cha sita uliotolewa mwaka 2014,uzito wa alama  katika gredi  A (1), B+ (2), B (3), C (4), D (5), E (6) na F (7).
“Katika mfumo wa jumla ya pointi , madaraja ua ufaulu hupangwa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne.Daraja I-III hubainishwa kwa idadi ya pointi alizopata mtahiniwa wakati daraja la Nne hubainishwa kwa kutumia kigezo cha mtahiniwa kafaulu angalu D mbili au C moja ama zaidi.
“Daraja la ufaulu wa mtihaniwa , kwa kidatoi cha nne hupangwa baada ya kupata jumla ya pointi alizopata katika masomo saba aliyofanya vizuri.
“Kwa mtahiniwa wa kidato cha Sita, daraja hupangwa baada ya kupata jumla ya pointi azilizopata katika masomo matatu ya tahasusi(Combination)
Kuhusu faida za mfumo mpya , alisema baraza linaona kuwa kutumia mfumo wa wastani wa pointi utawezesha kuwa na mfumo wa kutunuku matokeo wa aina moja katika ngazi zote za mafunzo kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu, matokeo yaliyo katika mfumo wa wastani wa pointi kwenye cheti yatarahisisha kazi ya udahili wa watahiniwa unaofanywa na TCU  na NACTE katika ngazi za juu  za mafunzo.
Pia mfumo wa wastani wa pointi ni rahisi kueleweka kwa wadau wa kada mbalimbali kwasababu hutoa tafsiri yenye kuonesha mtahiniwa aliye na GPA kubwa ndiye aliye na matokeo mazuri.
Pamoja na hayo, alisema baraza limeona ni vema likaendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu mfumo wa kutunuku matokeo ya mtihani wa kidato cha Nne na cha Sita.Nia ya baraza ni kuhakikisha wadau wanakuwa na taarifa sahihi na uelewa wa namna mfumo huo unavyotumika.

No comments:

Post a Comment