Naibu Waziri Masele
Na Benedict Liwenga-MAELEZO
14/08/2014.
NAIBU
Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele amewataka vijana nchini kupenda kujikita
katika masomo ya sayansi na teknolojia kama mihimili yenye kuleta maendeleo kwa
haraka ulimwenguni ili waweze kupata ujuzi na mitazamo katika sekta ya gesi
ambayo inakuwa kwa kasi kubwa nchini.
Mhe.
Masele ameyasema hayo jana wakati alipokuwa akifunga Kongamano la Tatu la Vijana
Wanasayansi Duniani lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius
Kambarage Nyerere, kongamano ambalo liliwakutanisha vijana toka nchi zaidi ya
46 ulimwenguni zikiwemo baadhi ya nchi za Afrika ambapo Tanzania ilikuwa
mwenyeji wa Kongamano hilo.
Mhe.
Masele ameeleza kuwa sayansi na teknolojia ndiyo mihimili mikubwa ya sasa
katika kuleta maendeleo ya haraka katika nyanja mbalimbali kwani mambo mengi hivi
sasa hutegemea sayansi na teknolojia.
Aidha,
Mhe. Masele amezitaja baadhi ya changamoto zinazozikabili baadhi ya nchi za
Afrika katika kupata maendeleo ni pamoja na kutowekeza katika sayansi na
teknolojia hali inayopelekea baadhi ya nchi nyingi kukosa wataalam wa kutosha
katika mambo ya sayansi na teknolojia, hivyo amezitaka nchi za Afrika kuwekeza
katika sayansi ili kuweza ili kubadilisha uchumi wa Afrika.
“Sayansi
na teknolojia huleta maendeleo makubwa hivyo nawapa moyo vijana muendelee
kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika mambo ya sayansi na teknolojia ili
muweze kuleta uchumui endelevu”. Alisema Masele.
Akizungumzia
kwa upande wa Serikali ya Tanzania, Mhe. Masele amesema kuwa serikali ya
Tanzania imewekeza nguvu zake kwa sasa katika kuendeleza sayansi ya afya kwa
kuanzisha Vyuo mbalimbali na kuwasomesha watanzania nchi mbalimbali za nje ili
waweze kwenda kupata ujuzi na kuwa wataalam na wakaguzi katika sekta ya gesi
pamoja na mafuta kwa lengo la kuja kuisaidia nchi yao.
“Wajibu
wetu kama Serikali tumeamua kwa makusudi kusomesha vijana katika nchi
mbalimbali ili wakaweze kupata elimu juu ya sayansi na teknolojia hasa katika
masuala ya gesi ili kupata wataalam na wakaguzi wa kutosha nchini ambao
watalisaidia taifa kuinua uchumi wake na hivi sasa serikali imeanzisha vyuo
mbalimbali nchini, program mbalimbali za mafunzo kwa watanzania, imetoa
ufadhili wa masomo kwa watanzania na imedhamini makongamano ya vijana ili
wapate fursa ya kujiendeleza.” Alisisitiza Masele.
Mhe.
Masele amempongeza Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo kwa
kazi kubwa anayoifanya katika Wizara yake na pia amewapongeza vijana
waliohudhuria katika kongamano hilo pamoja kuyapongeza Makampuni wadhamini wa
kongamano hilo na kuyataka makampuni hayo kuendelea kuwekeza pamoja na kulipa
kodi ili serikali iweze kukusanya mapato na wananchi wapate kunufaika na mapato
hayo.
Naye
Rais wa Vijana Wanasayansi Duniani (YES) Bw. Meng Wang amemshukuru Makamu wa
Rais wa Tanzania, Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Naibu Waziri steven
Masele kwa kuwaunga mkono vijana waliohudhuria kongamano hilo na kuonesha hali
nzuri ya ushirikiano baina ya serikali na vijana na amewaasa vijana kujikita
katika sayansi na teknolojia kama mihimili mikuu ya maendeleo duniani.
“Naishukuru
sana Tanzania pamoja na ujio wa Mawaziri wake katika kufanikisha kongamano hili
la vijana wanasayansi, nawashukuru pia wadhamini wa makampuni mbalimbali wa
kongamano hili pamoja na vijana kwa ujumla toka nchi mbalimbali duniani”. Alisema Wang.


No comments:
Post a Comment