Marekani imetuma washauri wa kijeshi kwenda eneo la wa-Kurdi, kaskazini mwa Iraq, waziri wa ulinzi Chuck Hagel amesema.
Wanamaji na wanajeshi wa vikosi vya operesheni
maalum watakadiria hali ya kibinadamu lakini hawatajishughulisha na
mapigano, afisa mmoja wa usalama wa Marekani amesema.Marekani imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wa kundi la taifa la kiislamu Islamic state (IS).
Wanamgambo hao wamelazimu maelfu ya watu kutoroka makwao.
"Hii si operesheni ya kivita,” Bwana Hagel alisema katika hotuba yake akiwa Camp Pendleton, California.
Walio kwenye jopo hilo la kufanya makadirio wamewasili katika mji wa Irbil kaskazini mwa Iraq .
"watafanya makadirio ya kina ili kubainisha tunapoweza kuendelea kutoa msaada,” Hagel alisema.
Washauri hao wataongezea ujumbe wa 250 wengine walioko Iraq tayari.
Shirika la Umoja wa Mataifa limesema kuwa maelfu ya raia, wakiwemo wafuasi wa kundi la Yazidi, wamezingirwa na wanamgambo hao katika Milima ya Sinjar, na wanahitaji usaidizi ili kuokoa maisha yao.
Marekani, Uingereza na Ufaransa wamekuwa wakifikisha msaada wao kwa wa-Yazidi walioko eneo la kaskazini mwa mlima Sinjar.
Ndege za Uingereza zimewasili Cyprus ili kufanikisha juhudi za kupitisha msaada kwa kusaidia ndege za mizigo za Hercules kutambua maeneo salama ili kupeana msaada.
Serikali ya Marekani imesema ndege zake zimefikisha vyakula takriban tani 100,000 na zaidi ya lita 123,000 za maji safi ya kunywa katika eneo hilo.
Operesheni ya hivi punde ilitekelezwa siku ya Jumanne.
Hayo yakijiri, mshambuliaji mmoja wa kujitoa mhanga alilipua eneo la ukaguaji karibu na maskani ya waziri mkuu wa Iraq aliyeteuliwa hivi majuzi, Haider al-Abadi, kule Baghdad.
Reuters imesema ilipata ripoti hizi kutoka kwa mashirika ya ulinzi na vyombo vya habari vilivyoko katika maeneo hayo.
Hakukuwepo na habari za majeruhi au vifo kufikia wakati huo.
Siku ya Jumatatu Rais wa Iraq alisihi bwana Abadi kubuni serikali mpya, ishara ya kupuuzilia mbali waziri mkuu anayemaliza muda wake Nouri Maliki.
Hatua hii imetekelezwa miezi kadhaa baada ya kuwepo mapigano ya ndani, ambayo wataalamu wanasema yalichangia Iraq kutoweza kukabiliana na wanamgambo wa taifa la Kiislamu (IS).
No comments:
Post a Comment