Na
Rose Masaka na Lorietha Laurence-MAELEZO
TANZANIA ni miongoni
mwa Nchi ambazo zimeweza kupunguza maambuzi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa asilimia
33.
Hayo yamesemwa leo
jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. William Lukuvi
wakati akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa 20 wa Kimataifa wa
Ukimwi Duniani uliofanyika Melbourne nchini Australia Julai mwaka huu.
Amesema kuwa hatua hiyo
imefikiwa baada ya Serikali kuanza zoezi la kuzuia maambukizi kutoka kwa mama
mjamzito kwenda kwa mtoto, na tohari kwa
wanaume hasa kwa jamii iliyokuwa haifanyi hivyo.
“Tohari zinaonyesha kwa
wanaume inapunguza maambukizi kwa asilimia 60 na wanawake asilimia 44. Tiba ya
UKIMWI kwa mama mwenye virusi vya UKIMWI inapunguza maambukizi mapya kwa mtoto
kwa asilimia 97 na tiba kwa watu wazima wa kawaida inapunguza maambukizi mapya
kwa asilimia 96,” amesema Lukuvi
Naye Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Dkt. Fatma Mrisho amesema kuwa sababu
zinazochangia maambukizi mapya ni pamoja na baadhi ya mila desturi potofu za
kitanzania ,ikiwemo ndoa za utotoni, kurithi wajane, wanaume kuwa na wanawake
wengi na kuogopa kupima afya.
Mkutano huo ulikuwa na
kauli mbiu iliyosema “Ongeza hatua katika juhudi zote za kuthibiti Ukimwi” ulisisitiza
mapambano dhidi ya Ukimwi yanahitaji njia mbalimbali ikiwemo ushiriki wa wadau
na umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za Ukimwi kutoka vyanzo vya
ndani ya nchi na taasisi.
Mkutano huo ulihudhuriwa
na wajumbe 11,200 kutoka katika nchi 146 ikiwemo Tanzania.

No comments:
Post a Comment