.
Msichana Jackline Lasway 'Pendo', akiwa na majeraha ya kuunguzwa na uji wa moto.
Na Mwandishi Wetu ,
Singida.
MSICHANA mmoja mkazi wa eneo la Minga Manispaa ya Singida amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wa tajiri wake wa dukani kutokana na kile kinachosadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Msichana huyo Jackline Lasway maarufu kwa jina la Pendo amelazwa wodi namba mbili katika Hospitali ya Mkoa wa Singida, huku akiwa na majeraha ya moto sehemu ya sikio la upande wa kulia na mgongoni.
Akizungumza kwa taabu katika wodi hiyo jana, Pendo alisema kuwa tukio hilo limetokea jana mchana wakati akiwa dukani kwa bosi wake aliyemtaja kwa jina la Charles Kamnde “Frarucha”.
Alisema akiwa anaendelea na kazi yake ya kuuza bidhaa mbalimbali dukani hapo gafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji wa moto na kumtaka kumwagia usoni.
Alisema aligeuka ili uji ule usimwagigikie usoni na ndipo ulimuunguza sikio la kulia na mgongoni ambapo baada ya mke wa bosi wake kumkosa uso alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.
“Mimi sikua na ugomvi naye wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani na kufanya hili tukio, maana kama ni kazi mi nafanya kulingana na maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale,” alisema.
Alisema katika kurupushani za kujiokoa asichomwe kisu hicho alifanikiwa kumkamata mkono mwanamke huyo na kupiga kelele ambapo watu walifika na kumwokoa.
Hata hivyo alisema alichukuliwa na bosi wake hadi kituo cha Polisi mjini Singida na kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu na kuletwa katika hospitali hiyo, ambako amelazwa huku akiwa na majeraha makubwa mgongoni.
Muuguzi wa zamu katika wodi namba mbili ya wanawake, Anna Sprian alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri, na anaendea kupatiwa matibabu ya majeraha ya moto aliyopata.
Kwa upande wake mmiliki wa duka hilo Chale Kamnde ‘Frarucha’ alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hayuko tayari kulizungumzia kwani maelezo aliyotoa binti huyo yanajitosheleza
Baadhi wa kinamama waliohojiwa kuhusiana na tukio hilo wameonesha masikitiko yao kutokana na hatua ya mwanamke huyo kumwagia uji msichana huyo.
Amina Ramadhani alisema hicho ni kitendo cha kinyama kwa binti mdogo kama huyo na kwamba kama aliona kuna mahusiano ya kimapenzi na mumewe angetumia busara na kumwondoa dukani na sio kumuunguza kwa uji wa moto.
Veronika Masawe alisema amesikitishwa na tukio hilo na kusema kuwa hakiendani na haki za binadamu kwa kuwa ni kumdhalilisha msichana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Geofrey Kamwela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment