TANGAZO


Monday, July 21, 2014

Wizara ya Nishati na Madini yavuka malengo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi

*Ni baada ya kufikia asilimia 36 ya wananchi wanaotumia huduma ya umeme 



Injinia Bengiel H. Msofe Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi (REA), akisoma majina ya vijiji vilivyopo katika mpango wa kupelekewa huduma ya umeme kupitia Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya pili katika kijiji cha MKENDA, Wilaya ya Songea vijijini Jumapili.
Menejawa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Bw. Francis Maze akitoa namba za simu kwa wakazi wa Kijiji cha Mkenda, kwa ajili ya kuwarahisishia pindi wanapotaka kujua hatua iliyofikiwa katika zoezi la kusambaza umeme vijijini, Wilaya ya Songea Vijijini, chini ya REA II, unaotarajiwa kukamilika Juni mwakani.
Meneja wa TANESCO, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Bi. Salome Nkondola, akitoa namba za simu kwa wakazi wa MKENDA.

Mkandarasi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA II), Sampath Somarathne, akitoa namba za simu kwa wakazi wa MKENDA.


ILANI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika sekta ya nishati imefikiwa mara baada ya asilimia thelethini (30%), ya Watanzania kufikiwa na huduma ya umeme.


Hayo, yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. SOSPETER MUHONGO, wakati wa ziara ya Mhe. Rais JAKAYA KIKWETE, yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa RUVUMA.


Mara baada ya kupata maelezo hayo Rais KIKWETE amesema kwa kuwa Sekta ya Nishati ni moja kati ya miradi inayowagusa wananchi wengi kila mahali, Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, Prof. Sospeter Muhongo ametakiwa kuwaeleza wananchi kila mara hoja inayohusiana na masuala ya nishati ya umeme pindi inapotokea.

Katika maelezo yake, Prof. Muhongo ameueleza umati wa wakazi wa kijiji cha MKENDA, Wilaya ya SONGEA vijijini, kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi isemayo ifikapo mwaka 2025, asilimia thelathini ya wananchi wawe wamefikiwa na huduma ya umeme, Wizara imesambaza umeme hadi kufikia asilimia thelathini na sita (36), mpaka sasa.


Hata hivyo Prof. Muhongo ameeleza kuwa mara baada ya kutimiza malengo hayo, Wizara ya Nishati na Madini imejiwekea malengo mapya ya kuhakikisha huduma ya umeme inasambaa kwa wananchi kwa asilimia 50, kabla ya mwaka 2025, hivyo, kuchangia katika kuiingiza nchi katika nchi za kipato cha kati kwani uwepo wa nishati ya umeme unachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi ya nchi, hivyo kupunguza umaskini kwa wananchi.


‘‘Umeme ni uchumi, umeme ni afya bora, umeme ni elimu bora, umeme ni ajira na umeme ni furaha”, Prof. Muhongo alisisitiza,

Muhongo amesema ifikapo 2025 angalau asilimia 75 ya wananchi wanapata huduma ya umeme kutokana na kuzalishwa kwa umeme mwingi zaidi ambao ziada itauzwa nje ya nchi.


Kutokana na ahadi aliyoitoa kwa wakazi wa MKENDA, waliowasilisha maombi yao kwa Rais, likiwemo suala la kupatiwa huduma ya umeme, Prof. Muhongo aliwahakikishia wakazi hao kufikishiwa huduma hiyo kabla ya Juni mwakani na kuwa taka Mameneja wa Tanesco wa Kanda, Mkoa na Wilaya kutoa namba zao kwa wananchi ili kurahisisha ufuatiliaji wa ahadi ya kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na kuvitaja vijiji vitakavyofikiwa na huduma ya umeme kupitia REA II.

No comments:

Post a Comment