TANGAZO


Friday, July 18, 2014

Wazazi jijini Dar es Salaam watakiwa kupeleka watoto wenye umri chini ya miaka 5 kupata matone ya vitamini A na dawa za minyoo

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadik akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu kuwataka wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya chanjo kwa ajili ya kupatiwa matone ya dawa za vitamini A na za minyoo.

Na Aron Msigwa – MAELEZO.
18/7/2014. Dar es salaam.
WITO umetolewa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam hususan wazazi wenye watoto  walio na umri chini ya miaka 5 kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A na dawa za Minyoo kwa kuwapeleka watoto wao katika vituo mbalimbali vya afya ili waweze kupatiwa dawa hizo kabla ya terehe 20 mwezi huu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki ametoa wito huo leo, jijini Dar es Salaam kufuatia zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A na dawa za minyoo  kwa vituo vyote vya kutolea huduma vya Serikali, binafsi na mashirika ya dini  vilivyoainishwa katika manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni kuelekea mwisho.

Amesema  zoezi hilo lililoanza tarehe 7 mwezi huu  ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati  wa Lishe wa Taifa  uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2013  kwa lengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji katika kuongeza hali ya lishe nchini. 

“Zoezi hili sio geni kwani ni utaratibu ambao sote tunaufahamu kuwa Serikali yetu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wa Afya huendesha zoezi huendesha zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A na dawa za Minyoo kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5 nchi nzima  kila mwaka” 

Amesema zoezi la utoaji wa dawa hizo ni muhimu kutokana na  miili ya watoto hao kuwa katika mahitaji makubwa ya vitamin A kutokana na mchango wake  katika ukuaji wa miili na akili kwa kuimarisha uwezo wa kinga zao dhidi ya magonjwa pamoja na kuimarisha uwezo wa macho. 

Kwa upande wake mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Grace Magembe akizungumza kuhusu zoezi hilo ambalo linafikia kilele chake tarehe 20 mwezi huu amesema kuwa ni vema jamii ikawa na mwitikio chanya kwa zoezi hili kutokana na umuhimu wake  kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5.

Amesema kuwa zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A huokoa maisha ya watoto kwani huwalinda na dhidi ya maradhi hatari kama vile Kuharisha, Surua na maradhi ya mfumo wa hewa.

“Kila mzazi anatamani kumuona mtoto wake anakua akiwa na afya njema, watoto wenye upungufu wa Vitamini A wapo katika hatari ya kuugua maradhi,kupata upofu na hata kupoteza maisha” Amesisitiza.

Aidha, amesisitiza kuwa dawa zinazotolewa katika zoezi hilo ni salama kwani tayari zimepitishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kuthibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Nawasihi wananchi mjitokeze kwa wingi katika zoezi hili kwa siku zilizobaki kwa kuwa zoezi hili tunaloliendesha ni salama”

No comments:

Post a Comment