Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Maifa la Kuhudumia wakimbizi nchini, Joyce Mends Colc,akihutubia wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Nelson Mandela iliyofanyika jana, duniani kote na hapa nchini imeadhimishwa katika shule ya watoto wenye mahitaji maalum na kudhaminiwa na Vodacom.
Ofisa Habari wa Kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini, Stella Vuzo,(kulia) akibadilishana mawazo na maofisa wa kampuni ya Vodacom, Matina Nkurlu na Gloria Mtui. Kushoto ni Ofisa wa Ubalozi wa Afrika ya Kusini, Nkhetheleni Mphohoni ,wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Nelson Mandela iliyofanyika jana, duniani kote na hapa nchini iliyoandaliwa na Ubalozi wa Afrika ya kusini nchini na kuadhimishwa katika shule ya watoto wenye mahitaji maalum ya Sinza, jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania.
Wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom wakishiriki katika kusafisha mazingira ya shule ya watoto wenye mahitaji maalum ya Sinza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Mandela iliyofanyika jana na kuadhimishwa shuleni hapo iliyoandaliwa na ubalozi wa Afrika ya Kusini nchini kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania.
Ofisa Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Gloria Mtui akishikiana na wanafunzi wanaosoma katika shule ya watoto wenye mahitaji maalum ya Sinza jijini Dar es Salam, kusafisha mazingira ya shule hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Mandela iliyoandaliwa na Ubalozi wa Afrika ya kusini nchini kwa ushirikiano wa Vodacom.
Baadhi ya wanafunzi wa wanaosoma katika shule yenye mahitaji maalum ya Sinza jijini Dar es Salam, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Nelson Mandela iliyoandaliwa na Ubalozi wa Afrika ya kusini nchini kwa ushirikiano na Vodacom Tanzania.
WAFANYAKAZI wa Ubalozi wa Afrika ya kusini nchini na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania jana, Julai 18, 2014 wameungana na taasisi na wananchi kutoka sehemu mbalimbali duniani katika kuadhimisha siku ya aliyekuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini aliyejitolea maisha yake kupigania na kuondoa vitendo vya ubaguzi wa rangi na unyanyasaji nchini humo,hayati Nelson Mandela.
Siku ya Mandela ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuadhimishwa tarehe ya leo kila mwaka na imekuwa ikiadhimishwa siku kama hii sehemu mbalimbali duniani ambapo taasisi mbalimbali hushiriki kufanya kazi za kujitolea kuhudumia jamii kwa muda wa dakika 67 kumuenzi kiongozi huyu aliyeleta mapinduzi makubwa yenye historia ya kipekee duniani.
Katika kuienzi siku hii ya leo,Ubalozi wa Afrika Kusini nchini ,Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom wameshiriki katika shughuli za kuhudumia jamii ambapo wamesafisha mazingira ya shule ya watoto wenye mahitaji maalum ya Sinza jijini Dar es Salaam ambapo pia wamegawa zawadi mbalimbali kwa watoto wanaosoma shuleni hapo.
Kaimu Balozi wa Afrika kusini nchini, Terry Govender alisema wanajivunia kuwa na kiongozi hodari kama Nelson Mandela ambaye alijitolea nusu ya maisha yake kupigana dhidi ya ubaguzi mchini Afrika Kusini na kuwaasa watu kufwata nyayo zake kwani ni mfano wa kuigwa duniani.
“Kama ilivyokuwa kwa Nelson Mandela, alitumia mda wake na nguvu zake kuhamasisha amani na usawa na kupigania haki za wanyonge, Mandela pia kupitia mfuko wa watoto aliouanzisha, aliamini kuwa watoto wote wanapaswa kufurahia kukosekana kwa njaa, unyonyaji, unyanyasaji na kutokuwa na makazi, hivyo ndio maana sisi tunashiriki kwa kuirudishia jamii kile tulicho nacho na kufurahi pamoja na hawa watoto”, alisema.
Akiongea juu ya kushiriki katika tukio hili muhimu,Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania,Matina Nkurlu alisema kuwa kampuni inaona fahari kubwa kushiriki na kutoa udhamini kwa tukio hili muhimu la siku ya kiongozi mashuhuri duniani mwenye historia ya pekee katika mapambano ya kutokomeza vitendo vya kufifisha haki za binadamu.
“Vodacom tunajivunia kushiriki katika shughuli za kijamii za kuadhimisha siku maalum ya kiongozi shupavu wa Afrika,hayati
Nelson Mandela, aliyejitolea maisha yake yote kupambana na vitendo vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika na kuhakikisha vinatokomezwa kwa njia ya amani”alisema Nkurlu.
Alisema mbali na kumuenzi hayati Mandela kwa kutokomeza vitendo vya ubaguzi,Vodacom inatambua mchango mkubwa wa kiongozi huyo alivyokuwa mstari wa mbele kuhudumia jamii na moja ya sera ya kampuni ya Vodacom ni kushiriki katika kazi za kuhudumia jamii.
“Kwetu Vodacom kushiriki katika shughuli za kijamii ni moja ya sera yetu hivyo siku hii ni muhimu kwetu kama kampuni na wafanyakazi wake wote na siku zote tutakuwa mstari wa mbele kushiriki na kusaidia katika shughuli za jamii.Alisema.
Hayati Nelson Mandela ambaye alifariki mwaka jana desemba atakumbukwa daima kwa ushupavu wake wa kutokemeza vitendo vya kibaguzi nchini Afrika ya Kusini na baada ya kustaafu aliendelea kuisaidia changamoto mbalimbali za kijamii kupitia taasisi ya Mandela Foundation.
No comments:
Post a Comment