Sunday, July 13, 2014
Rais Kikwete: Kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu kutategemea kukubaliana kwa Wabunge wa Bunge la Katiba
Na Alhadj Yusuph,Tanga
RAIS Jakaya Kikwete amesema kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu, kutategemeana na kukubaliana kwa wabunge wa Bunge la Katiba kupitisha ama mfumo uliopo wa serikali mbili ama tatu.
Akizungumza jana kwenye majumuisho ya ziara yake mkoani Tanga katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa, Rais Kikwete alisema katika ziara yake amekuwa akiulizwa njiani kuhusu kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa Oktoba mwaka huu.
Alisema kufanyika ama kutofanyika itategemea makubaliano ya wabunge wa Bunge la Katiba ambao walikutana kwa mara ya kwanza Aprili mwaka huu na kuibuka mivutano iliyowagawa huku wengine wakitaka serikali mbili na wengine tatu.
"Kama wabunge watakubaliana na mfumo uliopo wa serikali mbili, uchaguzi unaweza kufanyika na hili matayarisho yake yanaendelea kufanyika...Lakini kama watapitisha serikali tatu niwazi kwamba uchaguzi hautafanyika kwa kuwa serikali ya Tanganyika itaanza mchakato wa katiba yake" alisema Rais Kikwete.
Rais alisema ikipita serikali tatu serikali itaingia gharama kubwa kwa kuanza mchakato wa katiba ambayo pengine italazimu kuundwa kwa tume nyingine ya katiba pamoja na kugahramia tena fedha kwa ajili ya wabunge wa bunge la katiba la serikali ya Tanganyika.
"Wakiafikiana serikali mbili unaweza pia kuchelewa kufanyika ingawa matayarisho yanaendelea, lakini ikiwa ni serikali tatu itabidi iundwe tena tume ya Jaji Warioba (Joseph) kutafuta katiba ya Tanganyika yote haya itategemea busara za bunge hilo," alisema Kikwete.
Bunge la katiba ambalo liliahirishwa mwezi mei mwaka huu hadi mwezi ujao litakapoanza tena, lilisababisha mgawanyiko kwa baadhi ya vyama vya upinzani ambao wameanzisha Umoja wa katiba ya Wananchi (UKAWA) baada ya kususia bunge hilo katika wiki zake mbili za mwisho.
Wabunge hao wa Ukawa, walikuwa na madai kwamba wanataka rasimu iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya katiba, yabaki vile yalivyo hasa kuhusu mapendekezo ya muundo wa serikali tatu lakini wabunge walio wengi wanataka muundo wa sasa wa serikali mbili uendelee.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete ametoa agizo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashuari kuhakikisha wanatenga viwanja katika kipindi cha wiki mbili kutoka sasa na kuwapa Shirika la Nyumba nchini (NHC) ili wajenge nyumba za makazi.
Rais alitoa agizo hilo baada ya malalamiko ya shirika hilo kwamba wameomba viwanja katika wilaya karibu zote nchini kwa ajili ya kuendelea na zoezi lake la kujenga nyumba za makazi lakini halmashauri nyingi zimekuwa na urasimu na hivyo kuwakwamisha katika jitihada zake.
"Naagiza Halmashauri zitenge maeneo ya kujenga nyumbaza NHC na agizo hili nalitoa kwa nchi nzima maana haiwezekani halmashauri zinatenga maeneo kwa ajili ya mtu mmoja mmoja lakini hawa wanaoweka uwekezaji mkubwa wanafanyia urasimu, baada ya wiki mbili nataka mkurugenzi aliyekataa kutenga maeneo maana yake atakuwa hataki kazi,"alisema.
Rais pamoja na mambo mengine alilalamikia tatizo la watoto wa shule kushindwa kumaliza shule pindi wanapoanza kusoma hatua ambayo amewataka viongozi wa mkoa wa Tanga kuhakikisha wanasimamia na kuwa na suluhisho la kudumu la utoro na mimba mashuleni.
Rais Kikwete alianza ziara katika mkoa wa Tanga machi mwaka huu kwa kuzitembelea wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga mjini kisha Julai 8 mwaka huu alirejea kumalizia ziara yake hiyo kwa kuzitembelea wilaya za Kilindi, Lushoto, Mkinga na Pangani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment