Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kufungua rasmi jingo la ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Ruvuma leo mjini Songea.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na kaimu Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Bibi Mary Mosha wakifunua kitambaa katika jiwe la msingi wakati wa ufunguzi wa jingo la ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma leo. Rais Kikwete yupo katika ziara ya kikazi ya wiki moja mkoani Ruvuma. (Picha zote na Freddy Maro)
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini kuhakikisha kuwa kesi za rushwa dhidi ya
watu mbali mbali inazozipeleka mahakama zinakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa
kwa maana ya washitakiwa kukutwa na makosa.
Aidha, Rais Kikwete ameitaka Taasisi hiyo kuwa karibu na umma akisema kuwa
TAKUKURU na umma ni sawa na maji na samaki kwa sababu Taasisi hiyo haiwezi
kufanikiwa bila ushirikiano na umma.
Rais pia amesema kuwa Serikali yake inakusudia kutunga sheria ya kuwalinda
watoa habari kwa TAKUKURU ili kufanikisha zaidi kazi ya Taasisi hiyo.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi, Julai 17, 2014, kwenye siku yake ya
kwanza ya ziara rasmi ya siku sita mkoani Ruvuma ambako ameanzia ziara yake
katika Songea Mjini.
Katika siku yake ya kwanza leo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma
Kikwete, amezindua ghala kubwa la kuhifadhia chakula lililojengwa na Wakala wa
Taifa wa Kuhifadhji Chakula (NFRA), amezindua nyumba za bei nafuu ambazo zimejengwa
katika eneo la Mkuzo na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), amefungua rasmi Ofisi
za TAKUKURU za Mkoa wa Ruvuma na pia amehutubia mkutano mkubwa wa hadhara
kwenye Uwanja wa Majimaji wa Songea.
Akizindua ofisi hiyo ya TAKUKURU, Rais Kikwete ameipongeza Taasisi hiyo kwa
kazi nzuri ambayo imekuwa ikiboreka kila mwaka lakini akasisitiza kuwa wakati
umefika kwa TAKUKURU kufiksha mahakamani kesi zile ambazo zina nafasi kubwa ya
kutuhumiwa kukutwa na hatia. "ni vyema tuhakikishe kuwa kesi zinazokwenda
mahakamani zinakuwa na mpangilio mzuri na nafasi kubwa ya Serikali
kushinda kesi hizo."
Ameongeza Rais Kikwete: "Ni vyema pia kuwa pamoja na mafanikio
yote ya TAKUKURU ni lazima taasisi hiyo iongeze ushirikiano wake na umma.
TAKUKURU na umma ni sawa na samaki na maji kwa sababu kama ilivyo kuwa samaki
hawezi kuishi nje ya maji, hivyo hivyo TAKUKURU haiwezi kufanikiwa bila
ushirikiano na umma, bila kupata habari kutoka umma."
Ofisi hiyo ya TAKUKURU ya Mkoa wa Songea imegharimu sh. bilioni 1.18 na imejengwa
kwa kiasi cha miezi 20 ikiwa ni sehemu ya sera ya Serikali ya kujenga ofisi
tatu za mikoa kila mwaka ili kuondoa uhaba wa ofisi za kufanyika kazi za
Taasisi hiyo.
Kwenye uzinduzi za nyumba za NHC, Rais Kikwete ameambiwa kuwa katika eneo hilo
la Mkuzo, shirika hilo limejenga kiasi cha nyumba 18 za kuuza na zimejengwa kwa
gharama ya sh. milioni 676.
Rais Kikwete pia ameambiwa kuwa nyumba hizo zimejengwa katika kutekeleza
kaulimbiu ya NHC ya "Nyumba yangu, Maisha yangu" ambayo mpaka sasa
inatekelezwa katika mikoa 14. Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Januari mwaka
jana na unakamilika mwezi ujao, Agosti, 2014.
Nyumba hizo, ameambiwa Rais Kikwete, kuwa zitauzwa kwa gharama ya kati ya sh. milioni
33 na 44 bila kodi ya VAT lakini ambayo inaongezeka na kuwa kati ya milioni 44
na 52 kwa kutegemea ukubwa wa nyumba - kuanzia ya vyumba viwili hadi nyumba
vitatu. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake mkoani humo.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
17 Julai, 2014
No comments:
Post a Comment