*Akagua bei za vyakula
*Akagua shughuli mbalimbali za kimaendeleo
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihoji bei ya chaza katika soko la Wete. Mtungo mmoja wa chaza unauzwa shilingi 500.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihoji bei ya ndizi mbivu katika soko la Wete.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akitembelea soko la Qatar, Chake Chake Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihoji bei ya samaki katika soko la Mtemani Wete. Bei ya samaki hawa ni shilingi 1500 hadi 3000 kwa samaki mmoja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na mfanyabiashara za maboga katika soko Wete.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikagua bwawa la kufugia samaki la kikundi cha “Kichakaa si Shangi” cha Kiuyu Minungwini, Wilaya ya Wete Pemba. (Picha na Salmin Said, OMKR)
PEMBA 17/07/2014.
Na Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea haja ya kuwashajiisha
wakulima kulima kwa wingi mazao yanayopendwa zaidi na wananchi, ili kupunguza
mfumko wa bei hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akitembelea masoko ya
Chake Chake na Wete Kisiwani Pemba kuangalia bei za bidhaa mbali mbali zikiwemo
za matunda, Maalim Seif amesema licha na kuwepo bidhaa nyingi lakini bei zake
bado ziko juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi.
Amesema ili kupunguza
tatizo hilo, hakuna budi kwa wakulima kutoa kipaumbele kwa mazao yanayotumiwa
zaidi na wananchi katika kipindi cha Ramadhani yakiwemo ndizi, majimbi na viazi
vitamu, ili kuepuka kuagiza mazao hayo nje ya Zanzibar.
Hata hivyo Maalim
Seif amesema bei ya baadhi za bidhaa inaridhisha kisiwani Pemba ikilinganishwa
na Unguja, licha ya kuwepo bidhaa ambazo pia ziko juu kuliko Unguja, hali
inayotokana na upatikanaji wa bidhaa hizo katika maeneo husika.
Baadhi ya
wafanyabiashara katika masoko ya Wete na Chake Chake, wamesema wanalazimika
kuuza bidhaa hizo kwa bei ya juu kutokana na wao kuuziwa kwa bei ya juu kwenye
minada ya bidhaa hizo, ambapo baadhi yake zikiwemo viazi vitamu na majimbi
hutoka maeneo ya Tanga.
Wakati huo huo Maalim
Seif ametembelea Bwawa la kufugia samaki Kiuyu Minungwini, na kuelezea
kuridhishwa na maendeleo yaliyopatikana katika ufugaji wa samaki.
Amesema iwapo ufugaji
wa samaki utaendelezwa, utasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wengi
wanaomaliza masomo na kuongeza kipato chao.
Amefahamisha kuwa
wajibu wa serikali ni kuwajengea wananchi mazingira ya kuweza kujiajiri kwa vile haina uwezo wa kuajiri watu
wote, na kwamba wananchi wana wajibu wa kutumia fursa hizo zinazowekwa na
serikali kuweza kujiajiri.
Katika kuunga mkono
juhudi za wafugaji hao Maalim Seif ameahidi kuwanunulia mashine ya kuvutia
maji, ili kurahisisha uingizaji wa maji katika mabwawa hayo ya kufugia samaki.
Mapema akisoma risala
ya wana kikundi hao wa “Kichakaa si shangi”, Bi. Khadija Khamis amesema
wameamua kuendeleza kazi ya ufugaji wa samaki ikiwa ni kuitikia wito wa serikali kwa vitendo.
Amesema tangu
kuanzishwa kwa kikundi hicho cha ufugaji mwaka 1994, wamepata mafanikio makubwa
ikiwa ni pamoja na kuongeza mabwawa ya kufugia samaki kufikia manane ambapo
sasa wanajenga bwawa jipya la kitaalamu.
Akielezea maendeleo
ya ufugaji wa samaki, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdillahi Jihadi Hassan,
amesema jumla ya vikundi 144 vya ufugaji wa samaki vimeanzishwa Unguja na
Pemba.
Amesema kwa ujumla
vijana wamehamasika na wamekuwa wakiwashajiisha wafugaji zaidi kuendeleza ufugaji huo, huku
wakitoa taaluma kwa wafugaji ili kuleta ufanisi zaidi.
Ameongeza
kuwa Wizara yake ina mpango wa kununua boti mbili na kutoa mafunzo kwa wavuvi,
ili waweze kutekeleza mrango mkubwa wa uvuvi katika bahari kuu.
No comments:
Post a Comment