Daraja la Ruhekei lililozinduiwa rasmi leo na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete katika kijiji cha Mkaole wilyani Nyasa mkoani Ruvuma leo.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwapungia mamia ya wakazi wa mji Songea wakati alipoingia katika uwanja wa michezo wa Majimaji mjini humo ambapo aliwahutubia katika mkutano wa Hadhara. Rais Kiwete yupo katika ziara ya kikazi ya wiki moja mkoani Ruvuma kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo (Picha na Freddy Maro)
RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kamwe
Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano kati yake na Malawi kuhusu mpaka
kati ya nchi hizo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa
Tanzania haioni matinki ama busara yoyote kuingia vitani na nchi yoyote jirani
kwa sababu yoyote ile.
Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo kwa
Malawi na nchi nyingine jirani wakati alipohutubia mkutano wa hadhara
uliohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa mjini
Mbamba Bay, mji mkuu wa Wilaya mpya ya Nyasa, jana, Ijumaa, Julai 18, 2014. Mji
huo uko kwenye pwani ya Ziwa Nyasa.
Rais Kikwete ambaye alikuwa anasemea
juhudi za kutafuta ufumbuzi wa suala la mpaka kati ya Tanzania na Malawi, Rais
Kikwete amewaambia wananchi hao: "Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna
sababu ya vita. Laleni usingizi bila wasiwasi, Kuleni samaki wenu kwa sababu
Tanzania haioni busara ya vita."
"Tanzania haiwezi kutumia nguvu
kupata suluhisho la mvutano wa mpaka. Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo
hilo bila kutumia njia ya vita. Tanzania
haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya
madiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee bali kwa
mipaka yote ya Tanzania," amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia amewaelezea wananchi
juhudi ambazo zimekuwa zinafanywa na Tanzania kutatua tatizo hilo la mpaka
ikiwa ni pamoja na kuliomba jopo la Marais wastaafu kusaidia kutafuta jawabu la
mpaka kati ya nchi hizo mbili. Marais hao Joachim Chissano wa Mozambique,
Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini wanasaidiwa na jopo la
Kimataifa la mabingwa wa sheria katika kazi yao hiyo.
Rais pia amewahakikishia Wananchi wa
Wilaya ya Nyasa kuwa ahadi na mpango wa Serikali kununua na kuweka Meli mpya
katika Ziwa Nyasa uko pale pale na kwamba mipango inafanywa ya kuhamisha
chelezo cha kujengea meli kutoka Mwanza kwenye Ziwa Victoria kuipeleka Itungi,
Kyela, Mbeya ili kuanza ujenzi wa meli hiyo.
Rais ambaye katika Kampeni ya Uchaguzi
Mkuu Mwaka 2010 aliahidi ununuzi wa meli tatu za kutoa huduma katika maziwa
makuu ya Tanzania ya Victoria, Tanganyika na Nyasa amesema kuwa kiasi cha shilingi
bilioni 23 zimetengwa tayari kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Meli hiyo.
Amesema kuwa michoro ya Meli hiyo ya
Ziwa Nyasa imelazimishwa kubadilishwa kidogo kwa sababu ya ukweli kuwa Ziwa
hilo lina mawimbi makali na huchafuka mara kwa mara tofauti na Maziwa Victoria
na Tanganyika.
Rais Kikwete pia amewaambia wananchi
kuwa Serikali inaendelea na mipango ya kujenga Reli kutoka Mtwara hadi Mbamba
Bay ili kuzidi kufungua ukanda wa Mtwara na kuweza kubeba Chuma na makaa ya Mawe
kutoka Liganga na Mchuchuma, maeneo yaliyoko katika mkoa wa jirani wa Njombe na
Wilaya jirani na Nyasa ya Ludewa katika Mkoa huo wa Njombe.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara,
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku sita
katika Mkoa wa Ruvuma, Rais Kikwete alikuwa na shughuli nyingi katika Wilaya ya
Nyasa ambako amezindua Daraja la Ruhekei lililoko katika Kijiji cha Mkalole,
kilomita nane kutoka mjini Mbamba Bay.
Rais Kikwete amesema kuwa ujenzi wa
daraja hilo ambalo lina sehemu tatu limejengwa kisasa kabisa ikiwa ni
maandalizi ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga, Wilaya ya Mbinga kwenda
Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa.
"Ni kweli Mwaka 2005 wakati wa
kampeni ya Uchaguzi Mkuu nilishindwa kuvuka hapa kwa sababu daraja lilivunjika
lakini ujenzi huu wa kisasa ni kwa sababu tunajiandaa kujenga barabara ya lami
kuunganisha Mbinga na Mbamba Bay," Rais Kikwete
amewaambia Wananchi kwenye daraja hilo.
Rais Kikwete pia ameweka jiwe la msingi
la Ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya ya Nyasa katika kijiji cha Kilosa kilichoko
karibu na Mbamba Bay na amezindua usambazaji wa umeme katika vijiji vya Wilaya
ya Nyasa. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake Mkoani Ruvuma.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, - Dar es Salaam.
19 Julai,2014
No comments:
Post a Comment