Watumishi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, wakipita mbele ya Jukwa Kuu wakati wa Maandamano ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yaliyoanza leo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salam.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa
Umma, Hab Mkwizu akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo, kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salam.
Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika akizungumza wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, iliyoanza leo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam.
Baadhi ya watumishi wa Umma wakifuatilia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza leo, kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam.
Ofisa Habari wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Robi Bwiru akimueleza jambo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Wizara
hiyo, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, iliyoanza leo, kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es
Salam.
Baadhi ya wananchi wakipata maelezo kuhusu shughuli
zinazofanywa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki , wakati
walipotembelea banda la Wizara hiyo katika ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam leo. (Picha
zote na Hussein Makame-MAELEZO)
Hussein
Makame-MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Kapteni
Mstaafu George Mkuchika amesema kuwa Tanzania inashika nafasi ya pili kati ya
nchi tano za Shirikisho la Afrika Mashariki katika suala la Utawala Bora na
vita dhidi ya Rushwa.
Waziri Mkuchika amayasema hayo, wakati akizindua Maadhimisho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini
Dar es Salaam.
Alisema kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza, Serikali
ya Tanzania ilitangaza vita dhidi ya Rushwa na imekuwa ikiimarisha mapambano
dhidi ya adui huyo hadi katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya
Kikwete.
“Katika nchi za Afrika Mashariki suala la Utawala
Bora na Vita dhidi ya Rushwa, Tanzania tunashika nafasi ya pili, Rwanda ni ya
kwanza, ya tatu ni Uganda na ya nne ni Kenya” alisema Waziri Mkuchika.
Waziri Mkuchika alikuwa akizungumzia madai
yanayotolewa na baadhi ya watu hapa nchini kuwa Serikali ya Tanzania haina
dhamira ya kupambana na Rushwa.
Alikanusha madai hayo na kusema kuwa Serikali ya Tanzania
ina dhamira ya kupambana na Rushwa ndio maana imepitisha Sheria dhidi ya
Rushwa,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) ina matawi
kila mkoa na kila wilaya.
Alisema kiashiria
kingine cha kuthibitisha kuwa Serikali ya Tanzania inapamabana na Rushwa ni
kufikishwa mahakamani kwa watu wanaotuhumiwa na Rushwa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa mtumishi wa Takukuru
hawezi kuwafikisha watu mahakamani bila ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Hivyo aliwataka Watanzania wote kutambua kuwa wana
wajibu wa kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili
kufanikisha vita hiyo dhidi ya Rushwa.
Waziri Mkuchika aliwakumbusha Watanzania kuwa
mtumishi yeyote wa umma kumhudumia mwananchi ni haki yake, hivyo mtumishi
anayeomba Rushwa ili atoe huduma anashiriki katika tendo la Rushwa.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba watumishi
wajiepushe na Rushwa kwani Rushwa inawanyima watu haki, kukiwa na malalamiko
anayepata haki ni yule anayetoa Rushwa.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
ya mwaka huu inasema “Mkataba wa Misingi na Kanuni za Utumishi wa Umma Barani
Afrika ni Chachu ya Kuimarisha Utawala Bora na Uendeshaji wa Shughuli za
Serikali kwa Uwazi”.
No comments:
Post a Comment