Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim Seif Shariff Hamad, akitoa taarifa ya Chama kwa waandishi wa habari kuhusiana na Mkutano Mkuu wa Chama hicho unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 23/06/2014. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Massoud Hamad.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu za Chama hicho, Buguruni Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi kuu za Chama hicho Buguruni Dar es Salaam leo. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)
DAR ES SALAAM. 15/06/2014.
Na Hassan Hamad (OMKR)
CHAMA cha Wananchi (CUF), kinaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya Mkutano Mkuu Taifa utakaoambatana na uchaguzi wa viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu za Chama hicho Buguruni Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema maandalizi yote ya msingi kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika.
Maalim Seif amesema katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 hadi 27 mwezi huu, wajumbe wa mkutano watapokea taarifa mbali mbali za kazi za chama kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 ambapo pia watapata fursa ya kuzijadili.
Amebainisha kazi nyengine za mkutano huo kuwa ni pamoja na kuwachagua viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho ambao ni Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu.
Viongozi wengine watakaochaguliwa katika mkutano huo ni wajumbe wa Baraza Kuu la uongozi taifa pamoja na wajumbe wa viti maalum vya wanawake.
Maalim Seif amesema kwa sasa Chama hicho kinaendelea na vikao mbali mbali kikiwemo cha kamati tendaji, ikiwa ni maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mkutano huo ambapo wajumbe wote wa mkutano kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watakuwa wamewasili ifikapo tarehe 22/06/2014 kwa ajili ya mkutano huo wa kitaifa.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ameichambua bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2014/2015, na kusema kuwa ina mapungufu mengi.
Prof. Lipumba amewaambia waandishi wa Habari kuwa bajeti ikiwa nyenzo muhimu ya sera za serikali, inapaswa kuandaliwa kwa umakini ili iweze kutekelezwa kwa mujibu wa mahitaji yaliyopo.
Amesema ni jambo la kushangaza kuona bajeti inayoidhinishwa katika bunge kila mwaka haitekelezwi kama ilivyopangwa, na badala yake kunakuwa na tofauti kubwa kati ya bajeti inayoaishinishwa na ile inayopatikana kwa matumizi ya mwaka.
Amesema baadhi ya Wizara za Serikali zimekuwa zikipata fedha chini ya asilimia 50 ya matumizi yaliyopangwa, na kusababisha miradi mingi ya maendeleo kuzorota kutokana na ukosefu wa fedha.
Aidha amesema bajeti hiyo bado inabakia kuwa tegemezi kutokana na mapato ya ndani kuwa madogo ikilinganishwa na matumizi ya kawaida ya Serikali.
Prof. Lipumba amefahamisha kuwa serikali inapaswa kujipanga ipasavyo, ili kuepuka utegemezi kwa bajeti ya maendeleo ambapo amesema imekuwa ikitegemea zaidi misaada na mikopo kutoka nchi za nje na mashirika ya Kimataifa.
Ametaja mambo ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa utayarishaji wa bajeti kuwa ni pamoja na bajeti kuweza kufikia malengo ya uchumi mpana, ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, akiba ya fedha za kigeni pamoja na thamani sarafu.
Mambo mengine aliyobainisha ni ni kutaka matumizi yagawiwe kulingana na malengo ya sera ya taifa pamoja na kujenga mazingira ya utekelezaji mzuri wa bajeti.
Katika hatua nyingine Prof. Lipumba amesema bado bajeti hiyo haijaweka bayana juu ya ukuwaji wa deni la Taifa ambalo amesema limekuwa likikuwa kwa asilimia 20 kwa mwaka wakati ukuaji wa uchumi ni asilimia 7 kwa mwaka.
Amesema deni hilo ni hatari kwa Taifa na linapaswa kuwekewa mikakati imara ili lisiendelee kuongezeka na kudumaza pato la wananchi.
Amesema licha ya serikali kusema bajeti imelenga kupunguza gharama za maisha kwa wananchi, lakini wananchi walio wengi bado wanaona kuwa gharama za maisha zinaendelea kupanda kwa kasi kubwa kuliko takwimu zinazotolewa na serikali.
No comments:
Post a Comment