Marehemu Edward Kahurananga |
MWANDISHI na mtangazaji
wa habari wa siku nyingi, Bwana Edward Kahurananga, amefariki dunia hapo juzi
tarehe 17/6/2014 baada ya kuugua na
kulazwa kwa muda mfupi.
Marehemu Edward
Kahurananga alizaliwa tarehe 25 Desemba, 1949 katika wilaya ya Kibondo mkoani
Kigoma. Alihitimu elimu ya Sekondari mwaka 1968 katika Sekondari ya Livingstone
iliyoko mkoani Kigoma.
Katika uhai wake alisoma
vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi. Mwaka 1970 aliajiriwa
na Radio Tanzania Dar es Salaam kama Mtangazaji Msaidizi daraja la III. Alifanya
kazi katika ngazi mbalimbali katika
mikoa katika mikoa kadhaa nchini chini ya Radio Tanzania Dar es Salaam .
Baadaye aliteuliwa kuwa
Mhariri wa Habari Mkuu wa Radio Tanzania
Dar es Salaam kabla haijaunganishwa na Televisheni ya Taifa kuunda TvT ambayo
baadaye ilibadilishwa kuwa TBC. Mwaka
2004, Marehemu Edward Kahurananga alihamishiwa Idara ya Habari-MAELEZO kama
Afisa Habari Mkuu.Wakati ule Idara ya Habari ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu.
Tarehe 25 Desemba,
2009, Edward Kahurananga alistaafu kazi kwa mujibu wa kanuni za Utumishi wa
Umma wakati huo Idara ikiwa imehamishiwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo.
Edward Kahurananga alianza
kuugua akiwa Mwanza na kulazwa katika hospitali ya Bugando lakini akahamishiwa
hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambapo amefia tarehe 17 Juni, 2014 wakati
wakiendelea kujaribu kuokoa maisha yake.Atazikwa kesho (Ijumaa) tarehe 20 Juni,
2014 nyumbani kwake Vikindu jijini Dar es Salaam.
MUNGU
AIWEKE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI
AMINA
No comments:
Post a Comment