TANGAZO


Friday, May 9, 2014

Walimu Manispaa ya Dodoma waitaka Serikali kuboresha mafao na maslahi yao

Na John Banda, Dodoma.
WALIMU katika Manispaa ya Dodoma wameitaka Serikali kuboresha mafao na masilahi ya walimu kama ilivyo kwa kada zingine, ili kuondokana kwa kushuka kwa kiwango kikubwa cha ufaulu.
Ushauri huo, umetolewa na Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari ya Msalato, Dodoma, Dorah Sanga, kwenye Wiki ya Maadhimisho ya Elimu Kiwilaya  kutokana na shule hiyo, kupandisha ufaulu kwa mwaka 2013 na kuifanya kuwa ya kwanza katika Manispaa ya Dodoma mjini.
Maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika shule ya sekondari Umonga Dorah alisema kuwa kama kweli serikali inahitaji kuboresha sekta ya elimu itatakiwa kutatua kero ikiwemo hiyo ya viwango vya mishahara wanayolipwa kwa kuwa hakikidhi mahitaji yao hii ni pamoja na miundombinu kuifanya kuwa rafiki kwa upande wao.
Aidha alisema pamoja na changamoto hiyo serikali pia inatakiwa kufanya maboresho ya mazingira ya kufundishia na kujifunzia,ili kiwango cha ufaulu kiweze kufikia hadi asilimia 70 au zaidi  kwa malengo ya BRN kwa mwaka 2014.
“Kwa kweli serikali ikijidhatiti katika mahitaji muhimu kwa walimu ikiwa na kuongeza kiwango cha mshahara tunachokipata tofauti na watumishi wa sekta zingine ufaulu unaweza kuongezeka kwa kasi kubwa”alisema.
Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma mjini Robart Kitimbo akizungumza kwenye maadhimisho hayo aliwataka wadau wa elimu kuchangia sekta hiyo ili kuziboresha shule ili kuondokana na kero zinazowakuta walimu na wanafunzi.
Kitimbo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Lephy Gembe, alisema pamoja na walimu kudai haki zao,pia wadau wa elimu wanatakiwa kuangalia matatizo wanayokutananayo wanafunzi wa kike.
Alisema shule nyingi za sekondari hazina hostel suala ambalo limekuwa likiwasababishia wanafunzi hao kukosa ulinzi wa kutosha na kuwasababishia kupata mimba kunakutokana na kurubuniwa na wanaume.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amezitaka pia shule ambazo hazikufanya vizuri katika ufaulu zikiwemo za sekondari na msingi kuongeza juhudi na kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 70  ikiwemo na kuliangalia suala zima la wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti shuleni.

No comments:

Post a Comment