Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) Bruno Mteta akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio yaliyopatikana baada ya ongezeko la makusanyo ya mrabaha kwenye madini ya ujenzi kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Kushoto ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Ukaguzi kutoka wakala huo Mhandisi Liberatus Chizuzu.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwasikiliza maafisa kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) leo jijini Dar es Salaam. Wakala huo ulieleza mafanikio yaliyopatikana baada ya kuongeza makusanyo ya mrabaha kwenye madini ya ujenzi.
Mkurugenzi wa Udhibiti na Ukaguzi wa Uzalishaji wa Biashara ya Madini kutoka TMAA Mhandisi Liberatus Chizuzu akiwaeleza waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam mikakati iliyowekwa na wakala hiyo, ili kuongeza makusanyo ya mrabaha kwenye sekta ya madini hapa nchini. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Wakala huo Bruno Mteta.
ofisa Habari kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania Yisambi Shiwa akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu zoezi la kuwakamata wachimba madini ya ujenzi jijini Dar es Salaam wasiokuwa na vibali. Alieleza kuwa zoezi hilo limesaidia kupunguza wachimbaji holela ambao hukwepa kulipa mrabaha na kuharibu mazingira kwa kuchimba maeneo yasiyoruhusiwa.
Na Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI imekusanya
takribani shilingi bilioni 3 kutokana na
kuongezeka kwa makusanyo ya mrabaha uliotozwa katika madini ya Ujenzi
katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani katika kipindi cha Juni mwaka 2011 hadi
Novemba mwaka 2013.
Hayo yamesemwa
na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA) Bruno Mteta wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Mteta alisema
awali kabla wakala huo haujaanza ukaguzi wa madini ya ujenzi kiasi kilichokuwa
kikikusanywa ni shilingi milioni tatu tu kwa mwaka hivyo kwa sasa kiwango hicho
kimefikia wastani wa Bilioni moja kwa mwaka.
Alisema ukaguzi
umeimarishwa katika vituo vyote ambavyo wafanyabiashara wanaojihusisha na
biashara hiyo wanalazimika kupita na kuonyesha vibali vya kusafirisha madini
hayo ambavyo ni vocha maalum zinazotolewa na wakala huo ili kudhibiti wale
wanaokwepa kulipa mrabaha.
“Tumejipanga
vizuri kuhakikisha kuwa kila anayetakiwa kulipa mrabaha katika biashara ya
madini ya ujenzi anafanya hivyo kwa kuimarisha ukaguzi kupitia vituo vyetu vya
Afrikana, Pugu, Chalinze na katika maeneo yote yaliyobainishwa kutumika katika
uchimbaji wa madini ya Ujenzi” alisema
Mteta.
Katika hatua
nyingine Mteta alisema kuwa ni wajibu wa kila mchimbaji na mfanyabiashara wa
madini kulipa mrabaha unaostahiki ambapo kifungu cha 87 (6) cha sheria ya
Madini ya mwaka 2010 kinachotaka mrabaha ulipwe kwa kuzingatia thamani halisi
ya madini (gross value)yanapofikishwa sokoni au kwa mtumiaji.
Naye Mkurugenzi
wa udhibiti na Ukaguzi wa Uzalishaji na Biashara ya Madini Mhandisi Liberatus Chizuzu alitoa wito kwa wananchi hasa
wafanyabiashara wa madini ya ujenzi kuzingatia sheria na kanuni za Madini ili
kulisaidia Taifa kujenga uchumi imara.
Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Tanzania TMAA kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna Msaidizi
wa Madini Kanda ya Mashariki ulianzisha matumizi ya hati za mauzo ya Madini ya
Ujenzi katika ukaguzi wa uzalishaji na mauzo ya madini ya ujenzi Kanda ya
Mashariki (Mikoa ya Dar es salaam na Pwani) ambapo matumizi ya stakabadhi hizo
yameongeza pato la Serikali kwa kiasi kikubwa kutokana na makusanyo ya mrabaha
kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment