TANGAZO


Friday, May 16, 2014

Ujumbe wa Vijana walaani vitendo viovu vya kumvunjia heshima Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere


Mama Maria Nyerere afunguka 
*Aungana na Vijana kulaani vitendo viovu vya kumvunjia heshima Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere


Mama Maria Nyerere amezungumza na vyombo vya habari nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam leo na kuwataka vijana waliokwenda kumtembelea kuzunguka nchi mzima kuwaambia ukweli watanzania juu ya Maisha halisi ya mwalimu na mchango wake katika ujenzi wa Taifa huru la Tanzania.
Vijana wazalendo na wapenda Amani ambao wamemtembea Mama Maria wakiongozwa na Kiongozi wao anayejulikana kwa Jina la Mohamed Nyundo, wamesema wako pamoja na familia hiyo na kwamba wamesikitishwa na kampeni inayoendelea ya kumchafua Baba wa Taifa, kumkebehi na kumtuhumu kwa Uzushi na uzandiki.


KUMEKUWEPO na kampeni yenye nia ovu iliyoasisiwa hivi karibuni ya kuharibu taswira na heshima ya Baba wa Taifa Mwalimu Kambarage Nyerere katika jamii ya kitanzania na kimataifa. Kampeni hiyo inayoendeshwa na vibaraka wa nchi za magharibi na Ulaya, wazandiki na maadui wa Amani ya Tanzania imeendelea kusambazwa kwa kasi na kwa gharama kubwa.

Kutokana na kuwepo kwa Kampeni hiyo, jumuiko la Vijana Wazalendo na wapenda Amani  tumeamua kutoa tamko hili la kulaani na kupinga vitendo viovu vya baadhi ya watu kumtuhumu, kumkebehi na kumtukana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa kutambua Mchango wa Baba wa Taifa kama muasisi wa Taifa hili, mpigania Uhuru shupavu, Shujaa aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwa watu wake na kwa kutambua umahiri na jitihada za kujenga Taifa lenye Muungano, Umoja, Amani na Utulivu, jumuiko la Vijana wazalendo limeamua kuukumbusha Umma wa watanzania juu ya mchango wa utumishi uliotukuka wa Mwalimu Nyerere katika ustawi wa Taifa letu, lakini pia kuhamasisha watanzania hasa Vijana kuenzi kwa Vitendo moyo wa kujituma,weledi na busara za kiuongozi, pamoja na ushujaa na ushupavu wa Mwalimu Nyerere.

Sisi Jumuiko la Vijana wazalendo, tumeona ni vyema kuja kumfariji Mama yetu, Mama Maria Nyerere pamoja na familia nzima ya Mwalimu Nyerere na Kwamba sisi kama wananchi na Vijana makini tutaendelea kuwa pamoja na familia katika kupinga na kulaani vitendo hivyo viovu vya kejeli, matusi, tuhuma na kebehi zinazoelekezwa kwa Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa masikitiko makubwa, tumeshitushwa na kufadhaika kuona chombo kikubwa na taasisi muhimu ambayo ni muhimili mkubwa wa Serikali kama Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania linakuwa ndio uwanja wa matusi ya kumtukana muasisi wa Taifa hili, imetusikitisha na kutufedhehesha. Imefika wakati sasa, kwa Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudhibiti na kuondoa kinga yake kwa wale wote ambao kwa ujinga na kutumika wameamua kuanzisha na kuendesha kampeni kabambe ya kutia doa taswira na heshima ya Baba wa Taifa.

Imetolewa na:
Mohamedi Nyundo.
Kiongozi wa Jumuiko la Vijana Wazalendo na Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a Comment