Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kulia) akibadilishana hati ya mkataba wa msaada
wa sh. Bilioni 134 waliosaini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania leo jijini Dar
es salaam. Kushoto ni Balozi EU nchini Filberto Sebregond. (Picha zote na Wizara ya Fedha)
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania
imetiliana saini mkataba wa msaada wa zaidi ya Shilingi Bilioni 134 sawa na
Euro milioni 59.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kusaidia sekta ya kilimo na
usafirishaji nchini.
Mkataba huo ulisainiwa
na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile kwa niaba ya Serikali
ya Tanzania na Balozi wa EU nchini Filberto Sebregond leo jijini Dar es salaam.
Akizungumza baada ya
kutia saini mkataba huo, Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu ya msaada huo ambao
ni Shilingi Bilioni 82.4 ambazo ni sawa na Euro milioni 36.5 utatumika
kuendeleza sekta ya kilimo na kukuza uchumi nchini kwa kupitia kituo maalum cha uendelezaji kilimo ukanda wa
Kusini Tanzania (SAGCOT) na kuboresha miundombinu ya barabara za ukanda huo.
Vilevile Dkt. Likwelile
alisema kuwa sehemu iliyobaki ya msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 51.9 ambazo
ni sawa na Euro milioni 23 itatumika kuimarisha biashara na ushirikiano katika jumuiya
kwa kuanzisha kituo cha pamoja cha
ukaguzi mipakani (OSIS).
“Vituo hivyo vya
ukaguzi mipakani vitakuwa na manufaa si kwa Tanzania tu, bali hata katika nchi
mbalimbali zinazopakana na Tanzania” alisema Dkt. Lkwelile.
Alifafanua kuwa msaada
uliosainiwa unamanufaa kwa wananchi kwa kuboresha miundombinu vijijini na kusambaza
umeme vitu ambavyo vitasaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Naye Balozi wa EU
nchini Filberto Sebregond alisema kuwa anaamini msaada huo utasaidia juhudi za
Serikali ya Tanzania katika kuongeza nafasi za ajira, kupungua kwa bei za
bidhaa mbalimbali na kuendelea kukuza uchumi nchini.
Balozi huyo alisema
kuwa EU inaamini kuwa ushirikiano wake na Tanzania utaendelea kuimarika kwa kuhimiza
maendeleo kwa pande zote mbili na amani ya watu wake.
Hafla hiyo ya kusaini
mkataba ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha, Nishati na Madini,
Uchukuzi na Ujenzi, EAC, DFID, SAGCOT, wajumbe kutoka EU, Shirika la maendeleo
ya Ufundi kutoka Ubelgiji na washirika wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment