Mkurugenzi wa Ununuzi na Ushauri toka wakala wa huduma
ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Bw. Yoswam Nyongera
akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uwezo wa mfumo wa
kielektroniki utakaotumika kujaza mafuta katika magari na mitambo ya Serikali
ikiwemo kutunza kumbukumbu za malipo ya mafuta na hivyo kutoa mafuta kwa kadiri
ya fedha iliyolipwa na Taasisi husika. (Picha zote na MAELEZO)
Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI imeanza kutekeleza mradi wa kufunga mfumo wa
kielektroniki kujaza mafuta magari na mitambo ya taasisi za Umma ili kuongeza
tija katika utoaji huduma hiyo, kote
nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa wakala
wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Bw. Naftal Singwejo wakati wa mkutano na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Singwejo amesema mradi huo utashirikisha
Wizara,Taasisi zote za Umma,Wakala na Idara zinazojitegemea ambazo kwa mujibu
wa sheria ya ununuzi wa Umma na 7 ya Mwaka 2011 sura ya 410 kifungu cha 56 zinatumia
huduma hiyo toka kwa wakala huo.
“Hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu
zitahusisha kufungwa kifaa maalum (identification tag) katika mlango wa tanki
la gari au mtambo “alisema Singwejo.
Akizungumzia faida
za mfumo huo, Singwejo alisema hakutakuwa na mfanyakazi (Pump Attendant) wa
kuweka mafuta katika gari au mtambo na hivyo huduma hiyo itapatikana kwa haraka
na hivyo kuongeza tija.
Faida nyingine ni
kuwa taarifa ya matumizi ya mafuta ya chombo cha umma itapatikana kwa wakati
kwa njia ya mtandao na hivyo maamuzi sahihi kufanyika juu ya matumizi ya mafuta
kwa chombo husika.
Aidha, Singwejo alibainisha kuwa mfumo huo utaondoa
kabisa udanganyifu wa matumizi ya mafuta
katika magari na mitambo kwa taasisi za umma na kutoa nafasi kwa chombo
kilichodhibitika tu kuweza kupata huduma ya mafuta.
Naye Mkurugenzi Himili Biashara Bw. Malik Aram alisema
kuwa mfumo huo ni wa kisasa ambao unatumika katika nchi zilizoendelea na
majaribio ya mfumo huo hapa Tanzania yatafanyika katika kituo cha Kurasini
mwishoni mwa mwezi Julai, 2014 ambapo hadi sasa mfumo huo umeanza kusimikwa
katika kituo hicho.
Bw. Malik aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mfumo
huu katika kituo cha Mafuta cha kurasini katika mwaka huu wa fedha katika mwaka
ujao wa fedha mfumo huo utafungwa katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Mbeya,
na Mwanza.
Serikali ilianzisha wakala wa Huduma ya ununuzi
Serikalini (GPSA) ili kudhibiti matumizi ya fedha za umma yanayofanyika kupitia
ununuzi wa vifaa mbalimbali na mafuta kwa ajili ya magari na mitambo ya umma, hivyo mfumo huu ni moja ya hatua za
utekelezaji wa mpango huo kamambe wa kuwa na matumizi ya rasilimali za umma
wenye tija.
No comments:
Post a Comment