Hawa ni washiriki kutoka katika Halmashauri za Wilaya ya Mkalama, Ikungi, Manyoni, Manispaa, Iramba na Singida Vijijini wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi (katikati), na Watendaji kutoka Mamlaka ua Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), mjini Singida leo.
Na Hillary Shoo, SINGIDA.
MKUU wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi amehimiza Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kufanya kazi kwa kujituma na kutoa kwa wananchi taarifa kuhusu haki zao.
Mlozi aliyasema hayo leo, mjini hapa wakati akifungua semina ya uhabarisho kuhusu shughuli za Mamlaka ya usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii kwa viongozi na watendaji kutoka Halmashauri sita za Mkoa wa Singida.
Mwalimu Mlozi, alisema lengo ni kudhibiti waajiri wachache wenye tabia ya kuwarubuni na kupindisha sheria na kanuni wasipate mwanya wa kutimiza malengo yao.
Aidha alisema hatua hito itaifanya sekta hiyo ya hifadhi ya jamii kuwa endelevu na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la mtanzania, au ustawi wake.
“Sisi tulio karibu na wananchi hasa kupitia sekta isiyo rasmi kwa maana ya shughuli zinazofanyika kwenye maeneo yetu , ziwe kupitia vikundi hata mwananchi mmoja mmoja, ombio langu tuendelee kutoa elimu kuhusu manufaa ya kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa manufaa yao ya baadae.”.Alisema Mlozi.
Hata hivyo Mlozi alisema mamlaka hiyo (SSRA) mifuko inayosimamia kwa sehemu kubwa imekuwa ikihamasisha wananchi hawa walio kwenye sekta isiyo rasmi kupitia maonesho mbalimbali walipo Watanzania ili kujitangaza na kuwahamasisha wananchi zaidi kujiunga nao.
Alisema pia kuwa na lengo la kuiandaa jamii itakayofaidika na uwekezaji na uendelezaji mzuri wa mifuko ya hifadhi ya jamii kabla na wakati wa uzeeni.
Mapema Mjumbe wa Menejimenti na mkuu wa ununuzi wa (SSRA), Emanuel Urembo alisema faida ya kujiunga na mifuko hiyo ni kuwa na uhakika wa maisha ya baadae na kuiongezea serikali uwezo wa kinga dhidi ya watanzania ili kukuza uwekezaji nchini.
Urembo alisema mfuko huo ni ule wa kipensheni unaofuata misingi ya Kibima, kwa mwanachama kuahidiwa mafao ya aina mbalimbali pamoja na pensheni.
Aidha Mjumbe huyo alitoa ushauri kuwa kila mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi iwe ya kuajiriwa ama kujiajiri anatakiwa kujiunga na mfuko wowote wa hifadhi ya jamii autakao.
Pia alitaka kila mfanyakazi ambaye tayari ni mwanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii mara abadilishapo ajira anatakiwa kuendeleza uanachama katika mfuko wake wa awali wa Hifadhi ya Jamii (Mandatory Scheme).
No comments:
Post a Comment