TANGAZO


Monday, April 14, 2014

TBS na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Vedastina Justinian akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam kuhusu Mradi wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts), unaolenga kurahisisha taratibu za forodha, uhamiaji, usimamizi wa ubora wa bidhaa, ulinzi na usalama. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Miundombinu ya Kiuchumi Mhandisi Abdillah Mataka na kulia ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Mvungi.
Mkurugenzi Msaidizi Miundombinu ya Kiuchumi kutoka Wizara ya  Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhandisi Abdillah Mataka, akifafanua kwa waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo katika kujenga vituo vya utoaji huduma mipakani kwa kila nchi husika ili kurahisisha shughuli za utoaji huduma za forodha na uhamiaji. Ujenzi wa vituo hivyo, hapa nchini unafadhiliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo ya Japan. Kushoto ni Mchumi, Idara ya Biashara na Sekta za Uzalishaji kutoka wizara hiyo, Bw. Amedeus Mzee.
Mchumi Idara ya Biashara na Sekta za Uzalishaji kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Amedeus Mzee akizungumzia faida zitakazopatikana kwenye mradi wa vituo vya utoaji huduma kwa pamoja mipakani, aidha alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na watumishi wa vituo hivyo katika kuhakikisha mapato hayapotei kwa maslahi ya nchi yetu na jumuiya kwa ujumla. 
Mkurugenzi Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Tumaini Mtitu akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam mikakati ya kudhibiti ubora wa bidhaa za ndani na zinazotoka nje ili kuepuka madhara kwa watumiaji  wa bidhaa hizo. Kushoto ni Ofisa Uhusiano wa shirika hilo, Bi. Roida Andusamile.
Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mkutano wa Shirika la Viwango Tanzania uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Fatma Salum)

Na Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI imedhamiria kuwainua wajasiriamali wadogo hapa nchini ili kuongeza uzalishaji wa Bidhaa za ndani zitakazosaidia kuimarisha uchumi wa Taifa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shirika la viwango hapa nchini (TBS)  Tumaini Mtitu wakati wa Mkutano na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam.

Alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) kuwajengea uwezo wajasirimali wadogo ili hatimaye wazalishe bidhaa zenye ubora na hivyo kupata cheti cha ubora kinachotolewa na shirika hilo.

Mtitu aliongeza kuwa wajasiriamali wote wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa hapa nchini wanatakiwa kuthibitishwa na shirika hilo ili kuwalinda watumiaji wa bidhaa hizo kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa kwa mujibu wa  sheria.

Aliwataka Wajasiriamali hao kupitia SIDO ili waweze kujengewa uwezo wa kuzalisha bidhaa bora na baada ya hapo bidhaa zao ziweze kukaguliwa na kama zikikidhi vigezo wapate cheti cha ubora ambapo mchakato huo unaweza kuchukua mwezi mmoja.

Akizungumzia faida za Wajasiriamali kupata cheti cha ubora baada ya bidhaa zao kukidhi vigezo vilivyowekwa na shirikika hilo, Mtitu alisema unawawezesha wajasiriamali kupanua wigo wa soko la bidhaa zao na kuwa  wa kimataifa.
Wakati huo huo Mtitu aliwataka watanzania wote kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia shirika hilo ili waweze kupata cheti cha ubora  na kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.


Utaratibu wa kupata alama ya ubora ni kwanza kuwasilisha maombi kwa mkurugenzi Mkuu wa TBS, ukaguzi wa awali na upimaji wa Sampuli za bidhaa husika na hatimaye kutolewa kwa cheti cha ubora baada ya bidhaa husika kukizi vigezo.

No comments:

Post a Comment