Mzozo wa kidiplomasia unanukia kati ya Kenya na Somalia baada ya polisi kumkamata kimakosa mmoja wa maafisa wakuu wa ubalozi wa Somalia nchini Kenya Siyad Mohamud Shire .
Tayari balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Ali Nur ameitwa na serikali yake kueleza matukio yanayoambatana na kukamatwa kwa raiya wa asili ya kisomali ambao serikali inasema baadhi yao hawana vibali vya kuishi nchini.
Maafisa wa polisi nchini Kenya wamekuwa wakiendelea na msako wao dhidi ya wahamiaji haramu na wale wanaoshukiwa kushiriki matendo ya kigaidi na uhalifu.
Hata hivyo serikali ya Somalia imesikitishwa nao kwa kumkamata afisa wa ubalozi wa Somalia anayeshughulikia masuala ya kisiasa Siyad Mohamud Shire .
Kwa sababu hiyo Somalia imetuma taarifa katika vyombo vya habari ikisema kuwa waziri mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed amefanya mazungumzo na balozi wa Somalia nchini Kenya aliyefika Mogadishu hapo Jumapili kumweleza hatma ya raiya wa Somalia wanaoishi Kenya katika msako unaoendelea
Japokuwa serikali ya Kenya kupitia kwa wizara ya usalama wa kitaifa imekuwa ikishikilia kuwa hailengi jamii yoyote katika kuwakamata raiya wa kigeni na kuwarejesha katika nchi zao ama kambi za wakimbizi.
Taarifa hiyo imeanusha hilo na kusema maafisa wa polisi wamekuwa wakiwazuilia wasomali wengi na kuwatesa.
Tukio la kumnasa, Bwana Siyad Mohamud Shire limechukuliwa na serikali ya Somali kuwa ukiukaji mkubwa wa mkataba wa kidiplomasia.
Inasemekana kuwa bwana Shire alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa muda licha ya kuwa na kitambulisho cha kazi.
Mkutano kati ya waziri mkuu wa wa Somali na balozi wa Kenya ulifanyika baada ya baraza la mawaziri kuandaa kikao kisichokuwa cha kawaida kujadili hali ilivyo Kenya.
Juhudi za kumpata waziri wa mambo ya nje wa Kenya balozi Amina Mohamed kueleza msimamo wa serikali hazikufaulu ila maafisa wa polisi walikataa kuzungumzia suala hilo wakisema kuwa litashughulikiwa na ngazi ya juu.
Polisi nchini Kenya walianza msako kote nchini wiki tatu zilizopita baada ya matukio mengi yanayoambatanishwa na ugaidi ama uhalifu kutokea huku zaidi ya watu kumi wakifariki baada ya milipuko kadhaa kutokea katika mtaa wa Eastleigh na maeneo jirani jijini Nairobi.
Kisichojulikana kwa sasa ni namna nchi zote mbili zitakavyoendelea kushirikiana kidiplomasia katika mazingira yaliyopo.
No comments:
Post a Comment