CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga KIMELAANI
vikali kauli ya Mbunge James Lembeli Mbunge wa Jimbo la Kahama aliyoitoa kwenye
vyombo ya habari hivi karibuni iliyosema “CCM SIYO MAMA YANGU”.
Kwa hiyo Chama cha Mapinduzi Mkoa wa
Shinyanga na wana CCM wote kwa ujumla wamestushwa na kauli ya Mbunge Lembeli
anayetokana na CCM kwani kauli hii hatukutegemea sote kama
ingeweza kutolewa na Mwanachama ambaye tena ni Kiongozi ndani ya Chama.
Tunaomba ieleweke na tunautaarifu Umma na
wana CCM wote kuwa CCM haina tatizo kabisa na msimamo wa Mbunge James Lembeli
kuhusu msimamo wake wa serikali moja, mbili, tatu au nne na hata serikali ya Tanganyika
kwani huo ni uhuru wake binafsi. Tatizo
letu kubwa kwake ni kauli aliyoitoa kuwa “CCM SIYO MAMA YANGU” kwani kauli hiyo
ameitoa sio mahali pake na haihusiki na utashi wake binafsi katika msimamo
alionao katika BUNGE LA KATIBA. Kauli
hii inaukakasi na ni sawa na kukinajisi Chama.
Lakini jambo la ajabu na la kushangaza ni
kuhusu kulitumia jina la Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere vibaya, amekuwa
akijifananisha na kauli ya Baba wa Taifa tungependa atambue kuwa Lembeli hana
hadhi na sifa ya kujifananisha na Baba wa Taifa; kwani kujifafanisha kwake na
Baba wa Taifa huko ni matumizi mabaya ya kujitwisha sifa asizostahiki kwani
Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere alikuwa na karama, hekima na busara kubwa za
pekee na aliheshimika Dunia kote pia alikuwa anatoa kauli zake kutokana na
mazingira yaliyokuwepo wakati huo.
Kwani Baba wa Taifa kila jambo lililokuwa
linahusu swala la Chama na Mstakabali wa Taifa alitumia vikao kulizungumza sio
anavyofanya Lembeli kuropoka ovyo, kutumia ubabe na kukosa staha kwa Chama.
Tabia ya Mbunge Lembeli ya kukidhihaki Chama
imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, lakini tunapenda atambue na kumkumbusha kuwa
Lembeli hapo alipofika na jeuri yote na umaarufu alionao unatokana na CCM,
kabla ya mwaka 2005 hakuna Mtanzania aliyemfahamu popote nchini.
Lakini baada ya kupewa ridhaa na CCM na
hatimaye kuchaguliwa Ubunge ndipo akajenga umaarufu uliotokana na CCM. Lakini jingine tunapenda kumkumbusha kuwa
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Lembeli alikuwa na wakati mgumu sana ndani ya Chama
na nje ya Chama lakini Chama na Wanachama wakampigania kwa hali ya juu sana na
kwa mazingira magumu na hatimaye ushindi ukapatikana.
Leo shukrani anazotoa kwa Chama ni kukiambia
CCM SIO MAMA YAKE.
Basi na kama Lembeli anaona CCM SIO MAMA
YAKE ni vyema akatueleza MAMA YAKE NI NANI – KISIASA na kama
ana MAMA MWINGINE KISIASA ni VYEMA AKAMFUATA HUYO MAMA HUKO ALIKO anayeona
atamfaa kumpa umaarufu zaidi ya CCM.
Mwisho CCM Mkoa wa Shinyanga hakitakuwa
tayari na hakitawavumilia wanachama na viongozi wake wenye tabia kama ya Lembeli ya kuendelea kukidhalilisha Chama hadharani.
Lakini pia Chama kitaendelea kuheshimu
Demokrasia ndani ya Chama na Uhuru wa mawazo unaofuata maadili, miiko na
taratibu za Chama ndani ya vikao.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Taarifa hii imeandaliwa na Chama cha
Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga na imesomwa na:-
Ndugu
Emmanuel S. Mlimandago
Katibu
wa Siasa na Uenezi wa CCM
Mkoa
wa Shinyanga
05.04.2014
No comments:
Post a Comment