Msemaji wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bw. Richard Kasuga akiwaeleza waandishi wa habari, kuhusu tahadhari ya kutokea viwavi jeshi hapa nchini hivyo wananchi kutakiwa kuchukua tahadhari. Kulia ni Ofisa Habari wa Idara ya habari Maelezo, Frank Mvungi na kushoto ni Mkurugenzi Msidizi Afya ya Mimea,Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bw. Fabian Nkondo.
Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Mimea, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bw. Fabian Nkondo akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuwaelimisha wananchi kuhusu maboresho katika Sekta ya Kilimo ili kuleta Tija.
Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI imewatahadharisha wakulima nchini kuhusu
uwezekano wa kutokea kwa viwavi jeshi katika msimU huu wa kilimo.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Kilimo Chakula
na Ushirika Bw. Richard Kasuga wakati wa mkutano na vyombo vya habari leo
jijini Dar es salaam.
Akieleza Bw. Kasuga amesema ili kuhakikisha kuwa kazi
ya kukabiliana na viwavi jeshi inafanyika kwa umakini na ukamilifu wakulima
kote nchini wanahimizwa kukagua mashamba yao mara kwa mara ili kubaini dalili
za viwavi jeshi mapema hususani kwa mazao kama mahindi, mtama, uwele, ulezi, mpunga,
ngano na shayiri .
Akifafanua zaidi Bw. Kasuga amesema ni vyema wakulima
wanapaswa kutoa taarifa za awali pale wanapoona dalili za kuwepo kwa viwavi
jeshi kwa kuwasiliana na Maafisa ugani na kuzingatia ushauri wa kitaalamu
watakaopewa na kuupeleka kwa wakulima ambao ni walengwa.
Aliongeza kuwa Wakulima wamejengewa uwezo tangu 2008
ili kuweza kufanya utabiri kwa kuwapatia mafunzo na kusambaza mitego 374 ya
utabiri wa viwavijeshi sambamba na vipima mvua katika vijiji vya mikoa ya ya
Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Morogoro, Dodoma, Lindi, Pwani na Mtwara.
Bw. Kasuga vilevile alisema kuwa jumla ya lita 10,400 za viatilifu vya
udhibiti wa viwavijeshi vilisambazwa katika Makao makuu ya Kanda ambapo kanda ya Nyanda za juu Kusini (Mbeya)
lita 2000, Kanda ya Magharibi (Shinyanga) lita 1000, Kanda ya Kati (Dodoma ) lita
4,000 Kanda ya Kaskazini (Arusha) lita 2000 na Kanda ya Mashariki Dar es salaam
Lita 1,400.
Hadi mwezi Machi 2014 mlipuko ya viwavi jeshi imetokea
na kudhibitiwa katika mikoa 9 ambayo ni Mtwara, Lindi, Pwani, Mbeya, Morogoro, Dodoma,Tanga,
Arusha, na Kilimanjaro.
Aidha Kasuga alizitaka halmashauri za Wilaya kote nchini
kufuatilia mtandao wa mitego ya utabiri katika ngazi ya vijiji na kuwahimiza
watabiri wa vijiji husika kuendelea na kazi hiyo kwa msimu mzima wa kilimo.
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika inaendelea na
kazi ya kuratibu shughuli za kukabiliana na milipuliko ya viwavijeshi, kwelea
kwelea, nzige na panya katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
No comments:
Post a Comment