TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE (DENGUE FEVER)
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid
Utangulizi
Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa
kwa umma kuhusu kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue hapa
nchini. Ugonjwa huu ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususan hapa jijini Dar es
Salaam mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya wagonjwa
ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa
huu kwa kipindi hiki ni 70 ikiwa ni
wagonjwa 58 Kinondoni, 7 Temeke na 5 Ilala. Kwa kipindi cha wiki mbili
zilizopita idadi hii ya wagonjwa
imeongezeka mara mbili kuliko siku za nyuma. Vilevile kumekuwepo kifo cha mtu mmoja katika hosipitali ya
Mwananyamala.
Aidha, ugonjwa
huu si mpya hapa nchini kwani
uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni
2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na
ugonjwa ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172
walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni
ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi na madoadoa meupe
yenye kungaa.
Dalili za ugonjwa
huu ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa
hususani sehemu za macho, maumivu ya
viungo na uchovu. Dalili hizi huanza
kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14
tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya denge. Kwa wakati mwingine dalili za
ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi
wanaaswa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana
vimelea vya malaria ua dengue ili hatua stahiki zichukuliwe.
Vilevile mara chache mgonjwa anaweza kutokwa na damu sehemu za fizi,
mdomoni, puani, kwenye macho na pia njia ya haja kubwa na ndogo. Dalili hizi za
kutokwa damu pia zimeanza kuonekana hapa Dar es Salaam kwa wagonjwa watatu ambapo
mmojawapo alipoteza maisha.
Virusi vya homa
ya dengue vinaenezwa kwa binadamu baada
ya kuumwa na mbu aina ya “Aedes”. Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na
makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi
katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza
ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma zaidi wakati wa
mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi
kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine bila ya kuwepo na kuumwa na mbu
mwenye vimelea. Hadi
sasa hakuna chanjo ya homa ya denge. Mgonjwa
mwenye homa ya dengue anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa
huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Mgonjwa mwenye dalili za homa
ya denge anashauriwa kuwahi mapema kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili
kupata huduma stahiki kwani endapo
mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu anaweza kupoteza maisha.
Jinsi
ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
o
Kuangamiza mazalio ya mbu
ü
Fukia
madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
ü
Ondoa
vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo,
magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
ü
Fyeka
vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
ü
Hakikisha
maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
ü
Funika
mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
ü
Safisha
gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
o
Kujikinga
na kuumwa na mbu
ü
Tumia
dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”
ü
Vaa
nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
ü
Tumia
vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
ü
Weka
nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hivyo ni
jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa mazalio ya mbu yanaangamizwa na pia
kujizuia kuumwa na mbu.
Hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii
- Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga
Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na
Wakurugenzi.
- Ufuatiliaji wa homa hii ulianza kufanyika katika
Manispaa ya Kinondoni iliyoonekana kuwa na wagonjwa wengi zaidi ikafuatiwa
na Ilala na Temeke. Pia uchunguzi utaendelea
katika Mikoa na Wilaya nyingine tukianzia na zile wilaya zitakazoonekana
kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa.
- Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya
mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili
tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili
ziweze kuchukuliwa.
- Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kwenye vituo vya
kutolea huduma na mipakani kuhusu namna ya kutambua, matibabu na kujikinga
dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo
mgonjwa atapatikana.
- Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa
kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa, ambapo tunaendelea kupata
taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu
- Kutoa elimu kwa waandishi wa habari ili waweze
kuisambaza kwa jamii
- Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa dengue
uliopo kwenye vituo maalumu ‘Sentinel Surveillance Sites’
- Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili
kuweza kuthibitisha ugonjwa huu
- Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa
wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti
Hitimisho
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu bali wanashauriwa kwenda
katika vituo vya tiba mara mnapoona dalili.
Jamii inashauriwa kuhakikisha kuwa mazalio
yote ya mbu yanaangamizwa na pia kuzuia kuumbwa na mbu
Vilevile, wizara
inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri
wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia
na kudhibiti ugonjwa huu.
Mhe. Dkt. Seif
Suleiman Rashid (Mb)
Waziri – Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
25 Machi 2014
No comments:
Post a Comment