TANGAZO


Thursday, March 6, 2014

Wanafunzi watakiwa kuripoti vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia



Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Pindi Chana akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika Tarehe 8, Machi kila mwaka, Wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari leo Mjini Dodoma. Kulia ni Ofisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Bi. Jovina Bujulu.
Baadhi ya Waandishi waliohudhuria katika Mkutano wa Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana katika ukumbi wa Idara ya Habari leo, Mjini Dodoma. (Picha zote na Hassan Silayo)

Na Jovina Bujulu, Maelezo Dodoma
WANAFUNZI nchini wametakiwa kuripoti katika sehemu husika ikiwamo kwenye madawati ya kijinsia iwapo watakumbana na aina yeyote ya udhalilishaji wa kijinsia.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Pindi Chana wakati wa Mkutano na waandishi wa habari leo Mjini Dodoma.

Dkt. Pindi alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko kwa wanafunzi  hasa wa vyuo vikuu kukumbana na udhalilishaji wa kijinsia katika kipindi cha utoaji wa matokeo ya mitihani.

“Tumekuwa tukipata malalamiko sana kwa  wanafunzi wa hasa wa vyuo vikuu kukumbana na udhalilishaji wa kijinsia hasa katika kipindi cha matokeo ila wito wetu kwao ni kuripoti katika sehemu husika na Madawati ya kijinsia na sisi kama serikali tunaahidi kusaidiana nao kutokomeza tatizo hili”Alisema Dkt. Pindi.

Akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka Dkt. Pindi alisema kuwa dhumuni kuu la siku hii ni kuiwezesha jamii kupima utekelezaji wa maazimia, Matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za kimataifa zinazohusu masuala ya wanawake ili kuhakikisha haki za wanawake zinalindwa.

Aidha, Dkt. Pindi aliongeza kuwa wananchi hawana budi kuongeza juhudi katika kufichua, kubaini na kuchukua hatua za kukomesha ukatili na kunyimwa haki kwa wanawake kwani wanaofanyiwa hivi ni dada zetu, watoto wetu, mama zetu na wengine ni bibi zetu.

Maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika ngazi za Mikoa kwa kila mkoa kuandaa utaratibu wa maadhimisho haya na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia”

No comments:

Post a Comment