TANGAZO


Saturday, March 22, 2014

Wanafunzi wanawake Chuo cha Elimu ya Biashara Dar waweka historia

*Waanzisha Mfuko wa kuwakomboa kielimu

Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Mary Mwangisa (kulia) akizungumza jambo kabla ya kuanza kwa maandamano ya wanafunzi wa Kike wa chuo cha CBE kampasi ya Dar es salaam kuzindua  mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike chuoni hapo wenye lengo la kuwakomboa kielimu. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Taaluma ya Chuo hicho, Dkt. Ellen Oturu Okoedion. (Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO)
Waziri wa Wanawake wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE), Bi. Mwajuma Sangali akiwaongoza wananfunzi wa Kike wa chuo hicho wakati wa uzinduzi  wa mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kike, wenye lengo la kuwakomboa kielimu. 
Baadhi ya wanafunzi wa Kike wa Chuo cha CBE wakiwa wamebeba bango lenye ujumbe mahususi kutetea haki za wanawake na usawa wa kijinsia wakati wa uzinduzi wa mfuko maalum wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike wa chuo hicho.
 Wanafunzi wa Kike wa chuo cha CBE wakiwa kwenye maandamano kuelekea eneo la tukio.
Moja ya vikundi vya burudani cha Waswahili Classic Group cha chuo hicho, kikitoa buruduni wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfuko huo. 
Kikundi cha maagizo cha chuo hicho kikionyesha namna vitendo vya ukiukwaji wa maadili unavyodhibitiwa chuoni hapo na namna uongozi wa chuo hicho unavyowachukulia hatua za kinidhamu wanaokiuka maadili ya chuo hicho.
 Igizo la wanafunzi, wakiwa kwenye majadiliano chuoni hapo, bila kujali tofauti za jinsia.
Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Mary Mwangisa (kulia) akizungumza  na wanafunzi wa Kike wa chuo cha CBE kampasi ya Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa  mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike chuoni hapo wenye lengo la kuwakomboa kielimu.
Baadhi ya wanafunzi wa kike wa chuo hicho, wakifurahia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea wakati wa hafla ya uzinduzi wa  mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike chuoni hapo wenye lengo la kuwakomboa kielimu, kisiasa na kiutamaduni leo, jijini Dar es salaam.
Wanafunzi wa Kike wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Mary Mwangisa (katikati), wakati wa hafla hiyo.

Na Aron Msigwa – MAELEZO.
22/3/2014. Dar es salaam.

WANAFUNZI wanawake wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE) wamezindua mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya wanafunzi wa kike wenye lengo la  kumkomboa na kumwezesha mwanafunzi wa kike kujitambua, kielimu, kisiasa na kiutamaduni.

Akizungumza na jumuiya ya wanafunzi wa kike wa chuo hicho wakati wa uzinduzi  wa mfuko huo  leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Mery Mwangisa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema kuwa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo  ni ishara ya umoja na mshikamano wa wanafunzi wa kike chuoni hapo.

Amesema kuanzishwa kwa mfuko huo kunatokana na kuongezeka kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake pia  kukosekana kwa mifuko ya aina hiyo katika taasisi nyingi za elimu ya juu hapa nchini.

Ameeleza kuwa  malengo ya mfuko huo ni kumwezesha mwanafunzi wa kike wa CBE kujitambua kielimu, kisiasa na kiutamaduni na kuongeza kuwa yamekuja wakati muafaka kufuatia  mabadiliko yaliyopo sasa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

 Amefafanua kuwa mfuko huo ulioanzishwa katika chuo hicho ni fursa pekee ya kuwawezesha wanafunzi wa kike kunufaika kwa kupata elimu bora bila vikwazo.

“Napenda kutumia fursa hii kuushukuru uongozi wa chuo hiki kwa kuonyesha njia ya kuwajali wanawake na pia katika kuweka taratibu nzuri za kulinda maadili, katika maisha yangu sijawahi kusikia chuo kikuu chochote kimezindua jukwaa la wanawake lenye malengo mazuri kama yenu” Amesema Dkt. Mwangisa.

Ameeleza kuwa kwa muda mrefu wanawake kote nchini wamekuwa na juhudi  mbalimbali za kujikomboa kiuchumi pamoja na kulitumikia taifa kwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kwa ufanisi mkubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii pindi wanapokabidhiwa madaraka.

“Ninapowaangalia ninyi nafarijika maana naona viongozi wakuu wa serikali, naona marais na pia wakurugenzi wa biashara”

Akizungumza kuhusu kuanzishwa kwa mfuko huo na mafanikio yake  Dkt. Mwangisa amesema kuwa atatoa ushirikiano kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha kuwa mfuko huo unajengewa uwezo wa  kusimama na kuwanufaisha wanawake wanaokumbwa na changamoto zinazokwamisha maendeleo yao ikiwemo ukosefu wa fedha.

Amesema kuwa kukamilika kwa taratibu za jumuiya hiyo ikiwemo maandalizi ya katiba ya jukwaa hilo kutaliwezesha jukwaa hilo kupanga, kuandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kujiendesha ili kuwawezesha wanafunzi hao kutatua changamoto zinazowakabili kwa kulinda heshima yao katika jamii.

Kwa upande wake mjumbe wa Bodi ya Taaluma ya Chuo hicho Dkt. Ellen Oturu Okoedion amesema kuwa wanafunzi wa kike wa chuo hicho wanahitaji msaada kupitia mfuko huo utakaowawezesha kupambana na wimbi la wanafunzi wa kike kushindwa kumaliza masomo yao kwa kushindwa kumudu gharama za masomo.

Amewataka wanafunzi wa kike wa chuo hicho kutumia ipasavyo taaluma wanayoipata  kusaidia mfuko huo kupata fedha  ili uwe endelevu kwa maendeleo ya wanawake na chuo hicho.

“Ninyi mnasoma elimu ya biashara na ndio watalaam wenyewe sitarajii mfuko wenu ukose uwezo, naamini mtatumia taaluma yenu mnayoipata hapa chuoni kutafuta fedha kwa kuwa mnao uwezo huo” Amesisitiza Dkt. Ellen.

Naye Waziri wa Wanawake wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Bi. Mwajuma Sangali ameeleza kuwa wanawake kote nchini wana jukumu la kuandaa kizazi cha watu wenye upendo, uzalendo, kupenda kazi na maendeleo.

Amesema kuanzishwa kwa chombo hicho kunalenga kuboresha maisha ya wanawake hasa katika masuala ya elimu,jamii,uchumi na siasa.

No comments:

Post a Comment