Dk. Mamphela Ramphele kiongozi wa chama cha Agang, nchini Afrika Kusini
Mpango ambao ungekiwezesha chama kikuu cha upinzani nchini
Afrika Kusini cha Democratic Alliance (DA) kuwa na mgombea urais mweusi,
umevunjika.
Mpango huo uliofikiwa wiki iliyopita, ungeviunganisha vyama vya DA na Agang
cha mwanaharakati aliyepinga ubaguzi wa rangi Mamphela Ramphele.Muungano wa vyama hivyo ulionekana kuwa ungeleta upinzani mkubwa dhidi ya chama tawala cha ANC tangu kiingie madarakani mwaka 1994.
Bi Ramphele alikuwa mshirika na mzazi mwenzie wa Steve Biko, mpinzani mwingine mkubwa wa siasa za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, ambaye alifia katika mahabusu za polisi mwaka 1977.
Wachambuzi wa mambo wamesema muungano huo umeshindwa kukubalika miongoni mwa wapiga kura wengi weusi kwa sababu umeonekana kuwa chama kilichojaa wazungu.
Wafuasi wa chama cha DA walikuwa na matumaini kuwa Bi Ramphele angekisaidia chama kupata wapiga kura ambao hawaridhishwi na uongozi wa Rais Jacob Zuma na ANC, ambayo inaandamwa na kashfa za rushwa na kiwango cha juu cha umaskini miongoni mwa raia wa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment