TANGAZO


Thursday, February 13, 2014

Ubakaji 'ni jambo la kawaida' Somalia



Wengi wa wanawake wa Somalia hubakwa wakati wanapokimbia vita
Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limeitaka serikali ya Somalia kufanyia mageuzi sheria za taifa hilo ili kukabiliana na visa vingi vya ubakaji wa wanawake ambavyo vimekithiri nchini humo.
Katika ripoti yake yenye kauli mbiu 'ubakaji ni jambo la kawaida hapa' Human Rights Watch inasema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wanawake pamoja na wasichana nchini Somalia walikabiliwa na visa vingi vya ubakaji, dhuluma za kimapenzi kutoka kwa wanaume wakiwemo wanajeshi wa serikali katika mji mkuu Mogadishu.
Shirika la Human Rights Watch linasema kuwa wanawake pamoja na wasichana mjini Mogadishu wanaishi kwa hofu ya kila mara-serikali inayopaswa kuwalinda haijali.Taifa la Somalia bado linajaribu kubuni serikali thabibiti baada ya miongo kadhaa ya vita.
Mmoja wa waathiriwa aliyekimbilia nchini Kenya kwa jina Asha ameambia BBC kuwa alibakwa na wanaume wawili waliomstisha kwa bunduki.
Asha anasema alijaribu kutoroka ingawa hakufanikiwa kwani kila ya wanaume hao alimbaka kwa zamu baada ya kumlemea kwa nguvu.
Mwanamke huyo alifanikiwa kutoroka baadaye Somalia na kwenda katika kambi ya wakimbizi ya daadab nchini Kenya na hadi hivi leo bado anapata ndoto kuhusu kilichotokea siku hiyo.

Unyanyapaa


Waathiriwa wengi wa ubakaji hukaa kimya kwa kuhofia usalama wao
Tatizo moja linalowakabili waathiriwa wa ubakaji nchini Somalia ni unyanyapaa , hali ambayo huwapa ugumu wa kuongea ili waweze kupata kusaidiwa kimawazo.
Mtafiti wa shirika hilo Laetitia Bader alisema kuwa wanawake wamezoea kudhalililisha na wabakaji wao kwa sababu hawana matumaini ya kupata msaada wowote baada ya kubakwa.
Bader alisema kuwa umoja wa mataifa umekuwa ukijaribu kukusanya tarakimu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Tarakimu zilizokusanywa na umoja wa mataifa katika kipindi cha miezi sita ya kwanza- mwaka 2013 zilionyesha kuwa kulikuwa na visa mia nane vya ubakaji vilivyoripotiwa mjini Mogadishu kiwango ambacho ni kikubwa sana.
Bila shaka wanawake wengi hawajitokezi kutokana na unyanyapaa, kutokana pia na ukosefu wa habari kuhusu ni wapi wanaweza kutafuta msaada
Utafiti wa shirika la Human rights Watch uliangazia dhuluma dhidi ya wanawake wanaoishi katika kambi za wakimbizi katika eneo la Benadhiri mjini Mogadishu.
Ingawa shirika hilo linasema kuwa halikuweza kupata idadi kamili ya wanawake waliobakwa, tarakimu zilizotolewa na umoja wa mataifa zinaashiria kuwa tatizo hilo limeenea kwa kiwango kikubwa.
Shirika la Human Rights Watch linatoa mapendekezo ya kukabiliana na tatizo la ubakaji nchini Somalia likiitaka serikali kwa ushirikano na wafadhili wa kimataifa kubuni mikakati ya kupunguza visa vya ubakaji, kutoa msaada wa dharura kwa waathiriwa wa visa vya ubakaji na kubuni mikakati ya kudumu itakayozuia uhalifu huo katika siku za usoni.

No comments:

Post a Comment