Mbunge wa Jimbo la Chambani (CUF) kisiwani Pemba, Mhe. Yussuf Salim Hussein, akikabidhi pikipiki mbili kwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa ajili ya kuimarisha chama katika Wilaya za Kisarawe na Bagamoyo, mkoani Pwani jana.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi pikipiki mbili kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho (Bara), Julius Mtatiro, kwa ajili ya kuimarisha chama katika Wilaya za Kisarawe na Bagamoyo. Pikipiki hizo zimetolewa na Mbunge wa Chambani (CUF), Yussuf Salim Hussein. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)
DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewakumbusha viongozi wa majimbo kutekeleza ahadi wanazozitoa kwa wananchi, ili kujijengea uaminifu katika maeneo yao.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo jana katika Ofisi Kuu ya CUF Buguruni, baada ya kupokea pikipiki mbili kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Chambani Mhe. Yussuf Salim Hussein (CUF), kwa ajili ya Wilaya za Kisarawe na Bagamoyo.
Amesema kukabidhiwa kwa pikipiki hizo zenye thamani ya shilingi milioni tatu na laki mbili, kunaonesha jinsi mbunge huyo anavyofuatilia na kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, na kutaka viongozi wengine waige mfano wa mbunge huyo.
Mbunge huyo wa Chambani amekabidhi pikipiki hizo kufuatia ahadi aliyoitoa kwa wananchi wa Wilaya za Kisarawe na Bagamoyo, akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama hicho mwezi uliopita.
Akizungumza baada ya kukabidhi pikipiki hizo Mhe. Yussuf amesema ameamua kutekeleza ahadi hiyo kwa muda mfupi, ili kujenga matumaini ya wanachama kwa viongozi na chama chao.
Amesema ataendelea kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi katika maeneo mbali mbali, ili kuhakikisha kuwa chama hicho kinazidisha matumaini kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment