TANGAZO


Sunday, January 12, 2014

Rais wa Zanzibar, Dk. Shein akutana na Rais wa Muungano wa Comoro

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Rais wa Comoro, Ikililou Dhoinine, alipofika Ikulu ya Migombani, Mjini Unguja leo. Rais  wa Comoro alifika nchini kushiriki katika sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar, ambazo kilele chake kimefanyika katika Uwanja wa Amaan.
 
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akifuatana na Rais wa Comoro Ikililou Dhoinine, alipofika Ikulu ya Migombani Mjini Unguja leo. Rais  wa Comoro alifika nchini kushiriki katika sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar ambazo kilele chake kimefanyika katika Uwanja wa Amaan.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Rais wa Comoro Ikililou Dhoinine, alipofika Ikulu ya Migombani Mjini Unguja leo. Rais  wa Comoro alifika nchini   kushiriki katika sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar ambazo kilele chake kimefanyika katika Uwanja wa Amaan. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
 
ZANZIBAR na Visiwa vya Comoro zimesema zina kila sababu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yao kwa faida ya wananchi na Serikali za nchi mbili hizo. 
Hayo yamejitokeza wakati wa mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Rais wa Muungano wa Comoro Dk. Ikililou Dhoinine yaliyofanyika jana Ikulu ya Migombani Zanzibar.
Rais Dhoinine ambaye aliwasili nchini jana kuhudhuria maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi kufuatia mwaliko wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema anajisikia furaha kuwa miongoni mwa wageni walioalikwa kuhudhuria maadhimisho hayo kwa kuwa wananchi wa Comoro na Zanzibar ni ndugu na watu wenye historia ya karne nyingi ya ushirikiano.  
Alimueleza Dk. Shein kuwa Comoro na Zanzibar zina kila fursa za kujifunza kutoka kwa mwenzake kwa kuwa mbali ya historia inayofanana lakini pia zina mambo yayofanana ambapo kila upande una uzoefu ambao nchi nyingine inaweza kujifunza na kushirikiana.
Dk. Dhoinine alibainisha kuwa ipo haja ya kuufufua tena ushirikiano katika masomo ya dini ambao ulikuwa mkubwa kwa miongo mingi kati ya Comoro na Zanzibar huku akiafiki rai ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kutaka kuanzishwa ushirikiano katika elimu ya juu hasa kati ya vyuo vikuu kati ya nchi hizo.
Katika mazungumzo hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza Rais wa Muungano wa Comoro kuwa nchi mbili hizo zinaweza kushirikiana mbali na sekta ya kilimo ambayo mazao mengi yanayozalishwa nchini yanapatikana pia katika visiwa vya Comoro lakini pia katika sekta za utalii, uvuvi na biashara.
Halikadhalika Dk. Shein alibainisha kuwa sekta ya utamaduni na elimu ni miongoni mwa maeneo ambayo nchi mbili hizo zinaweza kushirikiana kwa kuanzia elimu ya juu ikiwemo ufundishaji wa lugha pamoja na Comoro kutumia vyuo vya elimu ya juu vya Zanzibar kusomesha wake. 
Kuhusu kuimarisha biashara kati ya Zanzibar na Comoro Dk. Shein alimueleza Rais wa Comoro kuwa Serikali ya Zanzibar imo mbioni kununua meli mpya ya kisasa ambayo itaweza kufanya safari kati ya nchi mbili hizo hivyo kuimarisha usafirishaji wa abiria na bidhaa. 

Dk. Shein alimuhakikishia Rais wa Muungano wa Comoro kuwa Tanzania inafanya kila jitihada kuimarisha uhusiano wake na nchi hiyo na kutolea mfano hatua ya Serikali ya Tanzania ya hivi karibuni kufungua Ubalozi nchini Comoro kuwa mojawapo wa jitihda hizo.
 
 
 

No comments:

Post a Comment