Rais Jakaya Kikwete |
Marehemu Dk. Mgimwa |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa
taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa, aliyekuwa pia
Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete amesema kuwa taifa
limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana
na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa
Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Kifo cha Mheshimiwa Mgimwa
kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi, 2014, na Katibu Mkuu
Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Katika tangazo lake, Balozi
Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya leo saa 5:20 (Saa za
Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic , Pretoria, Afrika Kusini
ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.
Balozi Sefue amesema kuwa
maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa yanafanywa na Serikali
kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi kuhusu suala hilo
zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.
Katika salamu zake kwa Waziri
Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu Mgimwa, Rais Kikwete
amesema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea
mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mgimwa.
Binafsi nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya
mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi
akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake
ilikuwa nzuri.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais
Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea
kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”
“Napenda kutoa pole nyingi na
rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao.
Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu
ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” amesema Rais Kikwete.
Rais pia amewatumia rambirambi
wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza mwakilishi na mtetezi
mahiri wa maslahi yao.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
01 Januari, 2014
No comments:
Post a Comment