TANGAZO


Friday, January 24, 2014

PINDA: Ujenzi wa Bomba la Gesi kukamilika mwaka huu



Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akizungumza katika moja ya mikutano yake.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi wa Bmba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kwamba anaamini kazi hiyo itakamilika mwaka huu kama ambavyo wataalamu wameamuahidi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Januari 24, 2014), wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba hilo la gesi lenye urefu wa kilometa 542.

Kwa mujibu wa Meneja wa mradi huo, Eng. Kapullya Musomba, kazi hiyo ilipangwa kukamilika Juni mwakani, lakini sasa hivi wanatarajia kazi hiyo itakamilika Desemba, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la Somanga-Fungu wilayani Kilwa, mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema jumla ya mabomba ya kutosha km. 440 yamekwishawasili nchini. “Hii ni sawa na asilimia 81 ya mabomba yanayohitajika kwa ajili ya kazi hii,” alisema.

Alisema kwamba kazi ya utandikaji wa mambomba hayo imefanyika vizuri kiasi kwamba km. 114 kati ya hizo zimekwishachimbwa (trenching) zinasubiri mabomba yaanze kutandazwa ardhini.

“Kwa kweli kazi inayofanywa ni nzuri, mabomba yaliyokwisha unganishwa mpaka sasa yanaweza kutosha kutosha km. 263 ambayo ni zaidi ya nusu.


Nina imani kwamba kazi hii itakamilika mapema kama alivyosema mshauri mwelekezi wa mradi huu,” alisema.

Mapema, akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Bomba, Eng. Thomas Baltazar alisema mabomba hayo yakishatandazwa ardhini yanaweza kudumu kwa miaka 30 lakini yakifanyiwa matengenezo na kuchekiwa mara kwa mara yanaweza kudumu kwa miaka 50.

Naye Mshauri Mwelekezi wa mradi huo, Eng, Peter Erasmus wa kampuni ya Worley Parson ya Afrika Kusini alisifu uimara wa mabomba yaliyotumika kwenye mradi huo na kumhakikishia Waziri Mkuu kwamba yana ubora wa hali ya juu ilikinganishwa na miradi mingine ambayo kampuni yake imesimamia katika bara la Afrika.

Waziri Mkuu alikagua hatua mbalimbali za ujenzi wa bomba hilo kuanzia Vikindu na Bungu mkoani Pwani; Somanga Fungu na Kitomanga mkoani Lindi ambako alionyeshwa uwekaji wa zege nje ya mabomba ili yasielee baharini; utandazaji wa mabomba ardhini na baharini na upindaji wa mabomba kwa kutumia mashine maalum.

Pia aliweka jiwe la msingi la Kiwanda cha Saruji cha Meis kilichopo eneo la Machole nje kidogo ya mji wa Lindi.

No comments:

Post a Comment