Msaidizi wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa anayeshughulikia
maswala ya haki za binadam, Ivan Simonovic, ameiambia BBC kuwa pande mbili
zilizo kwenye mgogoro nchini Sudan Kusini zimehusika katika utekelezaji wa
vitendo vya mauaji.
Bwana Simonovic amekuwa kwenye ziara ya maeneo mbalimbali ya Sudan Kusini ili
kupata ukweli kwa ajili ya kuandaa ripoti ya Umoja wa Matifa na ameelezea kuwa
ana ushahidi wa kutosha kusema pande mbili kwenye mgogoro zina hatia. Maelfu ya watu wameuawa katika mwezi mmoja uliopita katika mgogoro kati ya serikali na waasi wanaoongozwa na makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.
Bwana Simonovic aliambia BBC kwamba pande zote mbili serikali na waasi zilifanya uhalifu.
"Lakini kila upande ulihusika kwa kiwango fulani na katika maeneo tofauti. ''
Simonovic amesema kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi, yalikuwa Mji wa Bor kusini mwa nchi hiyo na Bentiu Kaskazini mwa nchi hiyo.
"Raia wapo kwenye kambi za wakimbizi wa ndani.Kinachochukiza ni kwamba kuna tatizo la ukabila hapa ambavyo mgogoro ulianza na nani anayewalenga raia.''
"Nadhani ni muhimu kuweza kuchunguza kwa undani chanzo cha mgogoro na pia kuripoti unyama unaotendewa raia.''
Bwana Simonovic amesema ripoti yake itakuwa tayari katika wiki chache zijazo.
Mgogoro huu ulizuka Disemba tarehe 15 wakati ambapo Rais Salva Kiir alimtuhumu aliyekuwa makamu wake wa Rais Riek Machar kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya serikali yake.
Inaarifiwa mgogoro wenyewe unaegemea zaidi upande wa ukabila. Bwana Kiir anatoka katika jamii ya Dinka yenye idadi kubwa ya watu huku Machar akitoka kabila la Nuer.
No comments:
Post a Comment