Na Frank Mvungi
Serikali yatumia zaidi ya shilingi Bilioni 16 kujenga Kampasi mpya ya Makao Makuu ya Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Chuo hicho Rosada Msoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam.
Rosada aliongeza kuwa kampasi hiyo imejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa ili kupanua wigo wa utoaji wa huduma bora katika sekta ya utalii.
Akifafanua zaidi alisema kuanzishwa kwa chuo hicho ni matokeo ya Kukua kwa Sekta ya Utalii nchini ambako kumepelekea kuongezeka kwa uhitaji wa watumishi wenye weledi katika fani za Ukarimu na Utalii.
“Tunaishukuru serikali ya Ufaransa kwa kuona umuhimu wa kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini kwa kuchangia katika ujenzi wa chuo chetu katika kampasi ya Bustani,ambayo ni makao makuu ya chuo chetu”alisema Rosada.
Aliongeza kuwa kwa mwaka 2012 jumla ya watalii 1,077,058 walitembelea Tanzania ukilinganisha na na wastani wa watalii 501,669 waliotembelea nchi yetu katika kipindi cha mwaka 2000.
Rosada alibainisha kuwa jukumu kuu la Wakala ni kutoa mafunzo bora katika fani za ukarimu na Utalii hapa nchini hali ambayo imechangia kukuza utalii nchini.
Naye Meneja wa Chuo hicho kampasi ya Temeke bw. Steven Madenge alisema kuwa chuo hicho kinaendelea na taratibu za kuhakikisha kuwa wahitimu wanaomaliza katika chuo hicho wanakidhi viwango vya kimataifa.
Chuo cha Taifa cha Utalii ni wakala pekee wa Serikali ulioanzishwa mwaka2003 kwa sheria ya wakala no. 30 ya mwaka 1997 kwa lengo la kutoa mafunzo ya Utalii na Ukarimu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment