TANGAZO


Sunday, December 15, 2013

CUF na madai ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, pamoja na mambo mengine, akimtakam Rais Jakaya Kikwete, kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ili kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. Kulia ni Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya.

Na Claudia Kayombo 

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakakuwa na jukumu la kusimamia ipasavyo mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba amesema kuridhiwa kwa hatua hiyo kutawezesha kuwepo maridhiano na mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki nyeti cha kukamilisha mchakato huo.

Prof. Lipumba ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari kwenye makao makuu ya chama hicho.

Alifafanua kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itawezesha kuimarisha utendaji kazi thabiti wa Serikali katika kupambana na ubadhilifu uliobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na Kamati za Bunge ianze kujenga utamaduni wa uwajibikaji na kutumia vizuri fedha za umma kwa maendeleo ya wananchi.

"Ili kusimamia vizuri mchakato wa kupata Katiba  Mpya na kuhakikisha kuwepo kwa maridhiano na mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki nyeti, ninamshauri Rais Jakaya Kikwete aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

"Jukumu kubwa la Serikali iwe ni kukamilisha mchakato wa kupata Katiba mpya, kuunda Tume Huru ya Uchaguzi, kuandikisha wananchi wote wanaostahili kupiga kura wapewe vitambulisho vinavyotumia alama ya mwili ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2015 unakuwa huru na wa haki,"alisema Prof. Lipumba.

Alisisitiza kuwa kura ya maoni kuhusu Katiba mpya haiwezi kuendeshwa kwa ufanisi bila kuwa na daftari la kudumu la wapiga kura linaloaminika.

"Kura ya maoni inabidi ipigwe na wananchi wa pande mbili za muungano, Tume ya Uchaguzi ya taifa inatumia Tume ya Zanzibar kuwa wakala na daftari la ZEC kubaini wapiga kura wa Zanzibar.

"Daftari la ZEC linawanyima wananchi wengi wa Zanzibar haki yakuandikishwa kupiga kura kwa madai kuwa hawana vitambulisho vya ukaazi, hivyo Tume ya Taifa itawajibika kuwaandikisha Wazanzibari hawa wapate haki ya kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba,"alisema.

Akifafanua alisema siyo kweli kwamba Katiba iliyopo hairuhusu kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwani inabainisha kuwa Rais anaweza kuteua Waziri Mkuu anayetoka katika Jimbo lolote la uchaguzi na wa chama chochote na kama ataungwa mkono na wabunge wengi anakuwa anapata wadhifa huo.

Prof. Lipumba alisema machakato wa Katiba mpya unapaswa kuwapa wananchi matumaini ya kujenga Tanzania yenye haki sawa kwa wote na itakayojenga uchumi ambao hatua, utaleta neema kwa wananchi wote.

Alisema Katiba mpya itamke wazi raslimali na maliasili ya nchi itatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote na vizazi vijavyo.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kupata Katiba ya mwaka 2015 una vikwazo vingi, ni wazi kuwa Katiba mpya haiwezi kupatikana ifikapo Aprili 26, mwakani wakati wa kusherehekea miaka 50 wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alibainisha kuwa kumekuwa na madai kuwa baadhi ya mawaziri ni mzigo kauli ambo imeungwa mkono na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nauye huku wengine wakidai kuwa Waziri Mkuu akiwa mzigo zaidi.

No comments:

Post a Comment