TANGAZO


Thursday, November 14, 2013

Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, azungumza na uongozi wa Wizara ya Biashara

*Aitaka kukabiliana na tatizo la bidhaa zilizokwisha muda katika soko la bidhaa nchini
 
Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko, wakiwa katika mkutano wa utekelezaji wa Mpango wa kazi za wizara hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ukumbi wa mikutano Ikulu, mjini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na uongozi wa Wizara  ya Bishara, Viwanda na Masoko, katika utekelezaji wa Mpango wa kazi
za wizara hiyo, ukumbi wa mikutano wa Ikulu, mjini Zanzibar leo. Kushoto ni Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (katikati), akizungumza na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za wizara hiyo, ukumbi wa mikutano wa Ikulu, mjini Zanzibar. Kushoto kwa Rais ni Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad. (Picha zote na Ramadhan Othman Ikulu)

Na Said Ameir, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kuongeza jitihada katika kukabiliana na tatizo la bidhaa zilizokwisha muda katika soko la bidhaa nchini.
Ameagiza kuwepo wa uangalizi wa karibu na wa mara kwa mara na kuongeza umakini katika ukaguzi wa bidhaa zilizomo katika soko pamoja na wakati bidhaa hizo zinapoingizwa nchini.
Dk. Shein ametoa kauli hiyo leo, wakati akihitimisha kikao cha kujadili taarifa ya Utekekezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 na robo mwaka ya mwaka wa fedha 2013/2014 ikiwa ni mfululizo wa vikao hivyo vinavyofanyika Ikulu.
“Lazima sheria zizingatiwe katika kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopitwa na wakati haziendelei kuwepo katika soko pamoja na kuangalia utaratibu wa kukagua ubora wa bidhaa kabla hazijashushwa bandarini ili kama hazikidhi masharti zisipewe fursa za kuingizwa nchini”Dk. Shein alisisitiza.
Sambamba na agizo hilo ameitaka pia Wizara hiyo kuongeza juhudi za kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini hususan za wajasiriamali wadogo wadogo wakiwemo wakulima wa chumvi nchini.
“Tuongezeni juhudi za kutafuta masoko ya bidhaa zetu ili kusaidia watu wetu”alieleza Dk. Shein na kusisitiza kuwa bidhaa kama chumvi haiwezi kukosa soko endapo Wizara itafanya jitihada za makusudi kuangalia masoko yakiwemo ya nchi jirani.
Kuhusu uimarishaji na kuwajengea uwezo wajasiiriamali nchini kupitia Programu ya Kurasmisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Dk. Shein aliitaka wizara kungalia namna bora ya kuhakikisha kuwa walengwa wa programu hiyo wanafikia malengo yaliyowekwa na hatimae kufaidika na programu hiyo.
Katika maelezo yake hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameipongeza Wizara hiyo kwa kutekeleza vyema malengo ya Wizara katika kipindi husika na kuongeza kuwa amevutiwa na mafaniko ya haraka ya Shirika la Biashara nchini ZSTC.
Wakato huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad amelipongeza Shirika la Biashara nchini ZSTC kwa kupata mafanikio ya haraka kufuatia mageuzi yaliyofanyika katika Taasisi hiyo muhimu kwa Zanzibar.
Maalim Seif ameeleza kuwa ametiwa moyo na mwamko mzuri wa utendaji pamoja na ubunifu wa Shirika hilo na kulitaka kuhakikisha kuwa linatambua umuhimu wa nafasi yake katika uhai wa Zanzibar.
Katika kukabiliana na tatizo la bidhaa kukaa sana katika soko na kufikia kumalizika muda wake Makamu wa Kwanza wa Rais alipendekeza kwa Wizara kukaa pamoja na waagizaji wa bidhaa nchini na kuwashauri kufanya utaratibu  ‘sale’ kwa kupunguza bei za bidhaa kabla hazijamaliza muda.
Mapema akizungumza kumkaribisha Katibu Mkuu kutoa taarifa ya utekekezaji wa Wizara Kaimu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko  ambaye pia ni Waziri wa Afya Juma Duni Haji alisema kuwa mwenendo wa bei ya bidhaa nchini umeendelea kuwa wa utulivu katika kipindi chote cha mwaka 2012/2013.
“Utulivu huo umetokana na hatua za kisera zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kutuliza makali ya hali ya maisha kwa wananchi wake”alieleza na kuongeza kuwa kumekuwepo na ziada ya chakula katika kipindi chote hicho.
Kuhusu uchumaji wa zao la karafu, Waziri alikieleza kikao kuwa msimu wa ununuzi wa zao hilo ulianza mwezi Julai, 2013 ambapo hadi tarehe 8 Novemba, 2013 jumla ya tani 1,992.4 za karafuu zilikuwa zimenunuliwa ikiwa ni asilimia 49.8 za makadirio ya tani 4,000 zinazotarajiwa kununuliwa kwa msimu wa mwaka 2013/2014.  
Kwa upande wa mauzo Waziri alieleza kuwa hadi tarehe 13 Novemba, 2013 Serikali ilikuwa imeuza nje karafuu tani 1,972 zenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 21.4.  

No comments:

Post a Comment