Na Aron Msigwa –
MAELEZO.
Uwezo wa Mapato na Matumizi ya Kaya
Binafsi nchini kwa mwaka 2011/2012, unaonyesha kuongezeka kutokana na
maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika sekta ya elimu, afya, umiliki wa
biashara, shughuli za kilimo, umiliki wa Vifaa na Rasilimali, makazi bora,
ongezeko la shughuli za kiuchumi na ajira.
Akitoa taarifa ya Utafiti
ulioendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuangalia tathmini ya kiwango cha
umasikini wa kaya kwa kutumia kipato na masuala mengine yasiyo ya umasikini wa
kipato leo, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacius
Likwelile amesema kuwa kukua kwa kiwango cha elimu, matumizi ya nishati ya
umeme, hali ya makazi na umiliki wa rasilimali ni miongoni mwa sababu za
kuongezeka kwa uwezo wa mapato na matumizi ya kaya.
Amesema kuwa utafiti huo ulifanyika
kuanzia mwezi Oktoba 2011 hadi Oktoba 2012 ambapo jumla ya kaya 10,186 kati ya
10,400 zilizokuwa zimelengwa zilihojiwa katika maeneo ya Dar es salaam na maeneo
mengine ya mijini na vijijini kwa Tanzania Bara.
Amesema uchumi wa Tanzania kwa sasa
umekua kutokana na kuimarika kwa sekta za ujenzi, usafirishaji, Elimu, shughuli
za mawasiliano, huduma za afya na huduma za kifedha.
“ Serikali imefanya mambo makubwa na
sasa uchumi wa Tanzania umekua kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa katika
kuboresha miundombinu ,kuwekeza katika sekta ya elimu, usafirishaji, mawasiliano
pamoja na ongezeko la huduma za kifedha” amesema.
Amesema kumekuwa na jitihada
mbalimbali zilizofanywa na serikali zikiwemo kuongeza ujenzi wa shule Zaidi hasa
zile za sekondari ambazo zimewezesha kupanda kwa kiwango cha wanafunzi
wanaojiunga katika elimu ya sekondari kutoka 15% mwaka 2007 hadi asilimia 29%
2011/12.
Amefafanua kuwa idadi ya kaya
zinazoishi katika nyumba zilizojengwa kwa vifaa vya ujenzi vya
kisasa, paa za kisasa, vigae na matumizi ya zege na kuta imara tangu mwaka 2007
imeongezeka kwa 66%.
Ameongeza kuwa matokeo ya utafiti
yanaonyesha kuwa asilimia 4% ya kaya zinamiliki pikipiki, 55% zinamiliki radio
na 57% ya kaya zote angalau mwanakaya mmoja anamiliki simu ya mkononi na
kufafanua kuwa kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo ya mengine ya mjini na
asilimi 88 ya kaya za Dar es salaam zinamiliki angalau simu moja ya
mkononi.
Katika hatua nyingine Dkt. Servacius
ameeleza wastani wa kiwango cha umasikini wa chakula kitaifa ni asilimia 9.7 na
kuongeza kuwa kiwango hicho kinafikia asilimia 11.3 kwa maeneo ya vijijini huku
Dar es salaam ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha umasikini wa chakula kwa
asilimia 1.0 na maeneo mengine ya mjini yakiwa na umasikini wa chakula kwa
asilimia 8.7.
Amesema miji mikubwa ina kiwango cha
chini cha umasikini wa chakula kwa asilimia 1.0 ambapo wananchi wanaoishi maeneo
mengine ya mjini wana umasikini wa chakula wa asilimia 8.7.
Ameongeza kuwa umasikini wa mahitaji
ya msingi kwa Tanzania bara ni asilimia 28.2 ikilinganishwa na asilimia 33.3 kwa
maeneo ya vijini na asilimia 21.7 kwa maeneo mengine ya mjini na kubainisha kuwa
Dar es salaam ina kiwango cha chini cha umasikini wa mahitaji ya msingi cha
asilimia 4.1.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa
Benki ya Dunia Bw. Richard Martini akitoa salaam za Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya
Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Phillipe Dongier, ameipongeza
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia vigezo vya tafiti vya kimataifa katika
kufuatilia hali ya umasikini na kipato nchini.
Amesema twakimu za utafiti huo
zilizotolewa zinaonyesha hali halisi ya maisha wanayoishi wanachi na kuongeza
kuwa zitaisaidia serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuelewa na
kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo na kukabiliana na changamoto za
umasikini zilizopo nchini.
Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacius Likwelile (katikati) akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu matokeo ya utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa. (Picha zote Aron Msigwa, Maelezo )
No comments:
Post a Comment